Ujerumani: Maelezo ya Saudi Arabia kuhusu mauaji ya Khashoggi hayakinaishi
Serikali ya Ujerumani imetangaza kuwa, maelezo yaliyotolewa na Saudi Arabia kuhusu mauaji ya mkosoaji wa utawala wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi hayatoshi.
Taarifa iliyotolewa jana na serikali ya Ujerumani ilisema kuwa, maelezo mapya ya Saudi Arabia kuhusu jinsi Jamal Khashoggi alivyouliwa hayatoshi wala hayakinaishi.
Taarifa ya serikali ya Ujerumani imeongeza kuwa, Saudi Arabia haijajibu maswali muhimu zaidi kuhusu mauaji ya mkosoaji huyo wa utawala wa kifalme wa Riyadh.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Saudi Arabia, Shalaan al-Shal'an alitoa taarifa Alkhamisi iliyopita akikiri kwamba, maiti ya Jamal Khashoggi ilikatwa vipande vipande baada ya kuuliwa na maafisa wa utawala wa nchi hiyo katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul huko Uturuki na kutolewa nje ya jengo la ubalozi.
Vilevile kwa mara ya kwanza kabisa al-Shal'an alifichua kwamba, mauaji hayo yalifanyika baada ya mabishano ya maneno, mapigano na kisha kudungwa sindano ya kupoteza fahamu na hatimaye kuuliwa Jamal Khashoggi.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alikuwa tayari amesema kuwa, serikali ya nchi hiyo imesitisha mikataba yote ya kuiuzia silaha Saudi Arabia hadi hapo baadaye.
Jamal Khashoggi aliuawa tarehe pili mwezi uliopita wa Oktoba baada ya kuingia katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki. Awali utawala wa Riyadh ulikanusha kuwa ulikuwa na habari kuhusu mahala alipo Khashoggi lakini baadaye ulikiri kwamba, maafisa wake ndio waliomuua mwandishi huyo wa bahari na kumkata vipande vipande.