Waziri Mkuu wa Uingereza katika jitihada za kusalia madarakani
Waziri Mkuu wa Uingereza ametangaza kuwa mazungumzo kati ya London na Brussels yatakuwa magumu zaidi iwapo Uingereza itambadili Waziri Mkuu wake.
Bi Theresa May kwa mara nyingine tena leo ameunga mkono mapatano ya sasa ya kujitoa nchi yake ndani ya Umoja wa Ulaya (Brexit) na kuyataja kuwa ni kwa ajili ya maslahi ya kitaifa ya Uingereza. Bi Theresa May amesisistiza kuwa mazungumzo ya siku chache zijazo yatagusia hasa suala la uhusiano wa baadaye kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya na hakuna mbadala uliowasilishwa hadi sasa kuhusu mapatano hayo ya Brexit.
Theresa May bila ya kuashiria moja kwa moja jitihada za baadhi ya wabunge wa Uingereza kwa ajili ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye amesema kuwa: Mazungumzo kati ya London na Brussels yatakuwa magumu sana iwapo Uingereza itambadili Waziri Mkuu wake.
Hii ni katika hali ambayo viongozi wa wanaounga mkono kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya wanaendelea kufanya mazungumzo ili kuchukua maamuzi ya kumuengua madarakani Bi Theresa May na nani anapasa kuwa mrithi wake iwapo watampigia kura ya kutokuwa na imani naye. Kushtadi hitilafu katika serikali ya Uingereza kuhusu mapatano ya Brexit khususan suala la mipaka ya Jamhuri ya Ireland na Ireland ya kaskazini katika siku za karibuni yamepelekea kujiuzulu viongozi kadhaa wa serikali ya London.