Wasaudia 18 wazuiwa kuingia Ujerumani kwa tuhuma za mauaji ya Khashoggi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imezuia kuingia nchini humo kundi moja la raia wa Saudi Arabia wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi aliyekuwa akiukosoa utawala wa Aal Saud.
Televisheni ya Russia Today imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumaini leo Jumatatu imewazuia kuingia nchini humo raia 18 wa Saudi Arabia kutokana na kutuhumiwa kuhusika katika mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa serikali ya kidikteta ya Saudia.
Tarehe pili Oktoba mwaka huu, Jamal Khashoggi aliuiliwa kikatili katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki.
Siku 18 baada ya mauaji hayo, na baada ya mashinikizo makubwa ya jamii ya kimataifa, hatimaye viongozi wa Saudi Arabia walikiri kuwa Khashoggi aliuliwa ndani ya ubalozi wake huo mdogo wa mjini Istanbul lakini hapo hapo wakadai kuwa aliuawa baada ya kutokea ugomvi wa kupigana ngumi kati yake na maafisa wa Saudi Arabia.
Riwaya hiyo ya viongozi wa Saudia ilipingwa na kila mtu hasa baada ya kupatikana ushahidi unaothibitisha kuwa kikosi maalumu cha mauaji kilitumwa katika ubalozi huo kwa ndege mbili maalumu kutokea Saudi Arabia kikiwa na zana kamili za mauaji.
Kashfa nyingine ni kwamba hadi leo hii viongozi wa Saudia wamekataa kusema wameupeleka wapi mwili wa Jamal Khashoggi. Hivyo viongozi wa nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa wanaendeleza mashinikizo yao dhidi ya ukoo wa Aal Saud huku kidole cha tuhuma kikielekezwa moja kwa moja kwa Mohammad bin Salman, mriti wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.