Russia: Nchi za Magharibi zisifikirie kuingilia kijeshi Venezuela
(last modified Wed, 30 Jan 2019 06:31:14 GMT )
Jan 30, 2019 06:31 UTC
  • Russia: Nchi za Magharibi zisifikirie kuingilia kijeshi Venezuela

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia jana usiku alizitaka nchi za Magharibi kuachana na mpango, fikra au dhana yoyote kwamba ipo haja ya kuingilia kijeshi huko Venezuela.

Sergei Ryabakov amesema kuwa Russia ipo tayari kikamilifu kutoa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa mazungumzo yanafanyika kati ya pande zinazozozana huko Venezuela. Viongozi wa Marekani  akiwemo John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House hivi karibuni alitishia mara kadha kuishambulia kijeshi Venezuela.  

Juan Guaido Jumatano iliyopita huku akiungwa mkono waziwazi na Marekani na waitifaki wake alijitangaza kuwa Rais wa Venezuela; hatua iliyotajwa na wananchi na serikali ya Venezuela kuwa ni mapinduzi dhidi ya Rais halali wa nchi hiyo Nicolaus Maduro. Marekani na waitifaki wake imekusudia kufanya mapinduzi nchini Venezuela kwa kumuunga mkono Juan Guaido spika wa bunge la Venezuela aliyefukuzwa kazi. Akthari ya nchi zikiwemo Iran, Russia, China, Cuba, Uturuki, Afrika Kusini na Uruguay zimelaani hatua hiyo ya Marekani na kusisitizia ulazima wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi ya Venezuela.  

Rais Nicolaus Maduro wa Venezuela

Venezuela miezi kadhaa iliyopita imekumbwa na ghasia na maandamano ya wapinzani wa serikali wanaofanya kila njama ili kuipindua serikali halali ya Rais Nicolaus Maduro. Wakati huo huo Washington inafanya kila iwezalo kuipindua serikali halali ya Venezuela kwa kuiwekea nchi hiyo vikwazo na kuwaunga mkono wapinzani wa serikali ya Caracas. 

Tags