Venezuela yanasa shehena ya silaha za Marekani
(last modified Wed, 06 Feb 2019 07:26:36 GMT )
Feb 06, 2019 07:26 UTC
  • Venezuela yanasa shehena ya silaha za Marekani

Vyombo vya usalama nchini Venezuela vimetangaza habari ya kunasa shehena kubwa ya silaha zinazoripotiwa kutokea Marekani, katika hali ambayo Rais Donald Trump amesisitiza kuwa serikali ya Washington itawaunga mkono kikamilifu wapinzani wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini, katika jitihada zao za kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Venezuela imesema shehena hiyo imenaswa katika bohari ya Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Arturo Michelena katika mji wa Valencia, na inaonekana kuwa imetumwa kutoka Miami, jimboni Florida nchini Marekani.

Miongoni mwa silaha zilizopatikana katika shehena hiyo ni bunduki 19, chemba za risasi 118, idadi kubwa ya risasi, simu za rununu 6 na radio ya mawasiliano 90.

Hapo juzi katika mahojiano yake na televisheni ya LaSexta ya Uhispania, Nicolas Maduro ambaye alikuwa akijibu matamshi ya Trump aliyesema kuwa kuna uwezekano nchi hiyo ikafanya mashambulizi ya kijeshi huko Venezuela, alimwambia rais huyo wa Marekani kwamba: "Unafanya makosa makubwa na utahitimisha kipindi chako cha urais kwa mikono iliyojaa damu." 

Rais Maduro akiwahutubia wafuasi wake

Mnamo tarehe 23 Januari, kwa baraka kamili za Marekani, Ulaya na baadhi ya nchi za eneo la Amerika ya Latini, Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela alichukua hatua kinyume cha sheria kwa kujitangaza rais wa muda wa nchi hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, katika mwaka uliomalizika wa 2018, wananchi wa Venezuela walishiriki kwenye uchaguzi na kumchagua kwa wingi mkubwa wa kura Nicolas Maduro kuwa rais wa nchi hiyo.

Tags