Russia yaionya Marekani isithubutu kuingia kijeshi Venezuela
(last modified Thu, 07 Feb 2019 14:51:19 GMT )
Feb 07, 2019 14:51 UTC
  • Russia yaionya Marekani isithubutu kuingia kijeshi Venezuela

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeionya Marekani kuhusu hatari ya chokochoko zake za kutaka kuivamia kijeshi Venezuela.

Katika taarifa yake ya leo Alkhamisi, Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imeionya Marekani isijaribu kuivamia kijeshi Venezuela kwani matokeo ya uvamizi huo yatakuwa ni maafa makubwa.

Taarifa hiyo ya Russia imesisitiza kuwa, ni wajibu wa Marekani kuelewa kwamba kuna machaguo mengine bora zaidi kuliko hilo la kuivamia kijeshi Venezuela.

Katika mahojiano aliyofanyiwa Jumapili usiku na televisheni ya CBS, rais wa Marekani, Donald Trump alitishia kuivamia kijeshi Venezuela na kusema kwamba kuingia kijeshi nchini humo ni moja ya machaguo yaliyoko mezani.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

 

Itakumbukwa kuwa, Rais Nicolas Maduro alishinda uchaguzi wa rais uliofanyika kidemokrasia mwezi Mei mwaka jana nchini Venezuela na kuidhinishwa kutawala nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka 6. 

Hata hivyo, tarehe 23 mwezi uliopita wa Januari 2019, na kwa baraka kamili za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya pamoja na baadhi ya nchi za eneo la Amerika ya Latini, Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela alijitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo suala ambalo ni kinyume kabisa na katiba ya nchi hiyo.

Nchi nyingi duniani ikiwemo Iran, Russia, China, Cuba, Uturuki, Afrika Kusini, Uruguay n.k, zinapinga vikali kitendo hicho kilicho kinyume na katiba ya Venezuela na uingiliaji wa madola ya kibeberu hasa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Tags