Maduro: Venezuela haihitaji msaada wa 'makombo' wa Marekani
(last modified Sun, 17 Feb 2019 04:37:02 GMT )
Feb 17, 2019 04:37 UTC
  • Maduro: Venezuela haihitaji msaada wa 'makombo' wa Marekani

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema ni kinaya kuiona Marekani inajidai kuwa ina hamu ya kuwapa wananchi wa nchi hiyo ya Amerika Latina kile inachodai kuwa ni msaada wa kibinadamu, katika hali ambayo imeiba mabilioni ya dola ya nchi hiyo kupitia vikwazo.

Akihutubia mkusanyiko wa wafuasi wake katika mji mkuu Caracas, Maduro amesisitiza kuwa nchi hiyo haituruhusu mashehena ya eti misaada ya kibinadamu kuingia nchini humo, huku Washington ikiendelea kuzuia mabilioni ya dola, pato la mafuta ya nchi hiyo.

Amesema: "Wameiba dola bilioni 30, kisha wanatupa chenga za mkate uliokauka eti ni msaada. Chakula hicho cha msaada kimeoza hatuna haja nacho."

Kadhalika Rais Maduro amelitaka jeshi la nchi hiyo kuimarisha doria katika mpaka wa nchi hiyo ya Colombia kwa lengo la kuzuia chokochoko zozote za Marekani. Ameongeza kuwa, Rais wa Colombia, Ivan Duque anapanga njama za kuishambulia Venezuela kwa msaada wa Marekani, lakini amesisitiza kuwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo viko tayari kuzima shambulizi lolote. 

Guaido (kulia) anayeungwa mkono na Marekani na baadhi ya nchi za EU

Itakumbukwa kuwa, Rais Nicolas Maduro alishinda uchaguzi wa rais uliofanyika kidemokrasia mwezi Mei mwaka jana nchini Venezuela na kuidhinishwa kutawala nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka 6. 

Hata hivyo, tarehe 23 mwezi uliopita wa Januari 2019 na kwa baraka kamili za Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya pamoja na baadhi ya nchi za eneo la Amerika ya Latini, Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela alijitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo, suala ambalo limepingwa vikali na aghalabu ya nchi duniani zikiwemo Iran, Russia na China.

Tags