Russia yamuonya, mpinzani wa Venezuela aliyejitangaza kuwa rais
(last modified Thu, 21 Feb 2019 07:53:40 GMT )
Feb 21, 2019 07:53 UTC
  • Russia yamuonya, mpinzani wa Venezuela aliyejitangaza kuwa rais

Serikali ya Russia kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Sargey Lavrov imemuonya Juan Guaidó, mpinzani wa serikali ya Venezuela aliyejitangaza kuwa rais wa nchi hiyo kwa hatua yake ya kuruhusu uingiliaji wa kigeni ndani ya taifa hilo.

Lavrov ametoa onyo hilo kutokana na Guaidó kuunga mkono uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi yake mwenyewe kupitia shehena ya misaada eti ya kibinaadamu kutoka Marekani na badala yake amemtaka mpinzani huyo wa serikali ya Venezuela kufanya mazungumzo na serikali. Ameongeza kuwa Russia inatiwa wasi wasi na vitisho vinavyotolewa na Marekani dhidi ya serikali ya Caracas na ambavyo kimsingi vinalenga kumuunga mkono Juan Guaidó kama ambavyo pia inapinga aina yoyote ya uingiliaji wa kigeni katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Raia wa Venezuela wakiendelea kuonyesha uungaji mkono wao kwa Rais Maduro licha ya njama za Marekani

Hii ni katika hali ambayo, kabla ya kuwasili nchini humo shehena ya Marekani eti ya kibinaadamu jeshi la Venezuela limepiga marufuku kuingia na kutoka meli zote katika bandari za nchi hiyo. Hii sio mara ya kwanza kwa serikali ya Russia kupinga aina yoyote ya uingiliaji mambo wa Marekani nchini Venezuela ambapo pia imeonya kwamba suala hilo litakuwa na matokeo mabaya. Kabla ya hapo pia Rais Nicolás Maduro sambamba na kumtaja Trump kuwa chanzo kikuu cha mgogoro wa Venezuela, alisema kuwa hatoruhusu misaada ya Marekani kuingia nchi hiyo na kufafanua kuwa, kuruhusiwa misaada hiyo kutaifungulia milango Washington ya kuingilia zaidi masuala ya ndani ya nchi yake. Aidha amefafanua kuwa, serikali ya Marekani inayopenda kujitanua inafanya kila iwezalo ili kuidhhibiti Venezuela. 

Tags