Marekani yadai siku za Maduro kuwa madarakani Venezuela zinahesabika
(last modified Mon, 25 Feb 2019 04:20:32 GMT )
Feb 25, 2019 04:20 UTC
  • Marekani yadai siku za Maduro kuwa madarakani Venezuela zinahesabika

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameonya kuwa, Washington itaendelea kuisakama na kuishinikiza serikali ya Venezuela hadi ifahamu kuwa siku zake za kutawala zinahesabika.

Mike Pompeo aliyasema hayo jana Jumapili katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Fox News na kuongeza kuwa, machaguo yote kuhusu kadhia ya Venezuela yako mezani.

Alipoulizwa kuhusu mpango wa Marekani wa kuivamia kijeshi nchi hiyo ya Amerikali ya Latini, Pompeo amesema "Marekani itafanya kile inapaswa kufanya."

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amekariri madai ya huko nyuma ya watawala wa Washington kwamba Rais wa Venezuela ni dikteta.

Hii ni katika hali ambayo, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesema kuwa serikali ya Caracas kwa ushirikiano na wananchi wa nchi hiyo watasimama kidete kupambana na madola ya kibeberu na hawatorudi nyuma katika suala hilo.

Rais Maduro akiwapungia mkono wafuasi wake mjini Caracas

Hivi karibuni, Maduro pia alizungumzia vitisho vilivyotolewa na rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu kuivamia kijeshi Venezuela na kusema kuwa uchunguzi wote wa maoni unaonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Venezuela wanapinga uingiliaji au vitisho vya kijeshi dhidi ya nchi yao. 

Haya yanajiri huku hali ya taharuki ikishuhudiwa nchini humo, baada ya malori yaliyokuwa yamebeba 'misaada ya kibinadamu' kutoka Marekani yakiteketezwa moto katika mpaka wa nchi hiyo na Colombia.

Tags