Mazungumzo ya Trump na Kim Jong-Un yafanyika Vietnam
(last modified Wed, 27 Feb 2019 16:21:59 GMT )
Feb 27, 2019 16:21 UTC
  • Mazungumzo ya Trump na Kim Jong-Un yafanyika Vietnam

Mazungumzo ya siku ya kwanza ya Kim Jong-Un, Kiongozi wa Korea Kaskazini na rais wa Marekani, Donald Trump, yamefanyika mjini Hanoi, Vietnam.

Kabla ya kuanza kikao hicho, Kim Jong-Un amesema kuwa, duru hii ya pili ya mazungumzo na Trump baada ya duru ya kwanza nchini Singapore mwaka jana, itakuwa na matumaini. Aidha ameongeza kwamba, katika mazungumzo hayo atafanya juhudi zake zote kwa ajili ya kufikiwa usalama na amani katika Peninsula ya Korea. Mazungumzo ya viongozi hao yataendelea hadi kesho Alkhamisi. Habari zinasema kuwa, Trump na Kim Jong-Un watafanya duru tano za mazungumzo kuhusiana na mzozo wa eneo la Korea. Viongozi hao waliwasili mjini Hanoi, Vietnam jana Jumanne. 

Baadhi ya silaha za nyuklia za Korea Kaskazini ambazo Marekani inataka ziangamizwe

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesisitizia udharura wa kutatuliwa mzozo wa Peninsula ya Korea kati ya Washington na Pyongyang.  Wang Yi ameyasema hayo leo mbele ya waandishi wa habari mjini Beijing ambapo sambamba na kuonyesha matumaini yake kuhusiana na mazungumzo kati ya Trump na Kim Jong-Un amesema kuwa kwa mara nyingine mazungumzo hayo yatasaidia kupiga hatua moja mbele kuelekea kwenye kutokomezwa silaha za nyuklia. Katika hatua nyingine serikali ya Japan imesisitiza kwamba itaendeleza vikwazo vyake vya kiuchumi dhidi ya Korea Kaskazini. Vyombo vya habari vya Japan vimewanukuu viongozi wa nchi hiyo wakisema kuwa, Tokyo itaendeleza vikwazo hivyo dhidi ya Pyongyang hata kama kutafikiwa makubalino katika kikao cha viongozi wa Marekani na Korea Kaskazini nchini Vietnam.

Tags