Uchunguzi: Wakristo wengi wamedhoofika kiimani kutokana na vitendo vichafu vya makasisi
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na gazeti moja la nchini Ujerumani umefichua kuwa, kashfa za kimaadili za viongozi na makasisi wa Kanisa Katoliki vimedhoofisha mno imani za Wakristo nchini humo na kuwafanya wapuuze kwenda makanisani.
Uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na gazeti la Bild la nchini Ujerumani unaonesha kuwa asilimia 82 ya Wakristo wa nchi hiyo wanaamini kwamba kashfa za kimaadili na vitendo vichafu vya viongozi wa Kanisa Katoliki vimetoa pigo kubwa kwa kanisa hilo na itachukua muda mrefu sana kufidia pigo hilo.
Uchunguzi huo unaonesha kuwa, asilimia isiyopungua 52 ya wafuasi wa Kanisa Katoliki wamekuwa wakifikiria kuachana kabisa na imani za kanisa hilo kutokana na vitendo viovu vya kingono na kijinsia vya makasisi na viongozi wa ngazi za juu wa kanisa hilo. Asilimia 32 wanafikiria kuachana kabisa na Ukristo na asilimia 22 wameachana kabisa na mafundisho ya dini hiyo.
Uchunguzi wa gazeti hilo unaonesha kuwa, udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya watoto wadogo na wanawake unaofanywa na makasisi ni moja ya matatizo makubwa yanayoitesa Vatican hivi sasa. Hivi karibuni Kanisa Katoliki la nchini Marekani lilisambaza majina zaidi ya elfu moja ya makasisi na viongozi wa kanisa hilo wanaokabiliwa na tuhuma za kuwadhalilisha kijinsia watoto wadogo.
Hadi hivi sasa kashfa za kijinsia imemlazimisha Papa Francis wa Kanisa Katoliki kuwavua uongozi idadi kubwa ya viongozi na makasisi wa kanisa hilo.
Wiki iliyopita, Kadinali wa Kimarekani ambaye pia alikuwa Askofu Mkuu wa Washingnton, Theodore McCarrick, alivuliwa cheo hicho na Papa Francis baada ya kupatikana na hatia ya kumdhalilisha kijinsia mtoto mmoja mdogo.