Kwa Nini Ndoto ya Marekani ya Kuwa Nchi ya Fursa Imeyoyoma?
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema, kutokana na “hali ya kijamii” ya Marekani inayozidi kuwa mbaya, haitazami tena nchi hiyo kwa jicho la mahala pa kuwashauri watoto wake wakasome au kufanya kazi.
"Leo mimi siwashauri watoto wangu waende Marekani wakasome au wakafanye kazi huko". Hiyo ndiyo kauli aliyotoa Kansela huyo wa Ujerumani, ambayo kwa hakika hatuwezi kusema ni indhari tu ya baba kwa wanawe. Hiyo ni ishara ya wazi ya kumalizika kwa zama; zama ambazo Marekani ilikuwa ikiitwa bila mjadala wowote "ardhi ya fursa".
Kinachojiri hivi sasa ni kugeuka na kubadilika taratibu, lakini kwa sura ya kina, ile nchi ambayo kuna wakati ilikuwa ndio kigezo cha dunia huru.
Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani, ameashiria nukta hii muhimu kuhusu kuyoyoma kwa ndoto ya Marekani, ambapo idadi ya Wamarekani hata wenye elimu kubwa wanaokabiliwa na tatizo la kupata ajira inazidi kuongezeka, ikiwa ni ithibati kwamba nchi hiyo sio tena “ardhi ya fursa” kama ilivyokuwa huko nyuma.
Merz, mwanasiasa mhafidhina ambaye kuna wakati alikuwa mkuu wa "Daraja la Atlantiki" na akafanya safari zaidi ya 150 za kuitembelea Marekani, sasa anawatahadharisha wanawe wa kiume wasiende kusoma na kufanya kazi upande huo wa pili wa Bahari ya Atlantiki. Mgongano huo unaoonekana waziwazi, chimbuko lake ni ukweli mchungu wa kwamba: Marekani ya Donald Trump sio tena ile ya zamani ya utoaji fursa na upokeaji watu. "Anga mpya ya kijamii" iliyopo, inaelezewa kuwa ni ya kikambi na mgawanyiko na isiyo na usalama, kiasi cha kuwarejesha nyuma hata waitifaki wa tangu na tangu wa Washington.
Hata hivyo, mabadiliko hayo ya mtazamo hayaishii kwenye sera za uhamiaji tu au za kuwaweka kizuizini watalii kiholela kunakofanywa na Idara ya Uhamiaji ya Marekani. Data za kiuchumi zinatoa taswira ya uhalisia zaidi ya soko la ajira la nchi hiyo. Kiwango cha vijana wasio na ajira wenye umri wa miaka 16 hadi 24 kilitarajiwa kufikia asilimia 9.5 mnamo mwezi Aprili 2026, na zaidi ya asilimia 41 ya vijana waliomaliza masomo wanafanya kazi ambazo hazihitaji shahada ya chuo kikuu. Benki ya Hifadhi ya Serikali Kuu imethibitisha kuwa, hicho ni kiwango cha juu zaidi tangu mwaka 2020. Kilichofanywa na ahadi ya Trump ya "muujiza wa ajira" ni kusababisha punguo la fursa milioni 6.9 za kazi.
Soko la ajira la Marekani hususan kwa kizazi kipya, halina tena ile nguvu ya mvuto ya huko nyuma. Akili Mnemba inafuta ajira za programu na za masuala ya fedha. Makampuni yanapunguza gharama, na bajeti za utafiti katika vyuo vikuu vya wasomi wenye vipawa zinapunguzwa kwa kiwango kikubwa. Hata taasisi za masuala ya hali ya hewa zinafungwa, na mzozo kati ya Serikali na Chuo Kikuu cha Harvard, ambacho ni nembo ya urazini wa kiakademia, umefikia kwenye kilele. Katika msimu uliopita wa mapukutiko, idadi ya wanafunzi wapya wa kigeni nchini Marekani ilipungua kwa asilimia 17, kiwango kikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 1948.
Ujerumani, ambayo ni kitovu cha uchumi wa Ulaya, inayahisi waziwazi mabadiliko hayo. Idara ya Taifa ya Utalii ya Ujerumani imeripoti kupungua kwa asilimia 14 safari za kuelekea Marekani zilizofanywa mwezi Aprili, huku wamiliki wa mahoteli nchini Marekani kuanzia Los Angeles hadi New York wakikiri kuwa, idadi ya wateja wao kutoka Ujerumani imepungua mno kuliko ilivyotarajiwa. Asilimia 65 ya wanaotaka kwenda kufanya kazi nchini Marekani wanataja sababu mbili kuu zinazowakwamisha, ambazo ni vizuizi vya upataji viza na wasiwasi wa kijiopolitiki. Wanaosafiri kwa ajili ya biashara, walezi wa watoto, na hata wahadhiri wa vyuo vikuu, hivi sasa wanafadhilisha kuelekea maeneo mengine. Gazeti la Washington Post liliripoti hivi karibuni kuwa, karibu nusu ya vijana wanaohitimu masomo nchini Marekani hivi sasa wanafanya kazi ambazo hazihitaji shahada ya chuo kikuu, huku ajira za taaluma za ngazi ya chini zikipungua sana.
Wakati huo huo, kasi ya kuwaachisha kazi wafanyakazi wa kiidara katika sekta kama vile teknolojia, fedha na utoaji huduma katika makampuni imeongezeka, sambamba na kukubalika utumiaji wa Akili Mnemba na upunguzaji gharama katika makampuni.
Kansela Merz wa Ujerumani si sauti pekee iliyoashiria kuyoyoma kwa Ndoto ya Marekani. Yeye ni sauti ya kizazi kipya tu cha wanasiasa wa Ulaya ambao hawawezi tena kufumbia macho changamoto za ndani ya Marekani. Ukosoaji wake kwa Trump wa "kutokuwa na mkakati katika vita dhidi ya Iran" na kudhalilishwa Marekani na Jamhuri ya Kiislamu ni kielelezo cha uelezaji mambo kinagaubaga ambao haukuwepo wakati wa muhula wa kwanza wa urais wa Trump. Tusisahau kuwa, mnamo mwaka 2019 alipohutubia katika chuo kikuu cha Harvard, Merz mwenyewe aliwahamasisha wanafunzi kwa shauku kubwa "waelekee Marekani kwa sura ya umiminikaji".
Lakini lugha yake hivi sasa imebadilika, yakiwa ni matokeo ya mabadiliko katika maoni ya umma nchini Ujerumani.
Pamoja na hayo, utegemezi wa kijeshi wa Ujerumani kwa Marekani ungali ni mkubwa. Pentagon imebakisha wanajeshi 31,000 wa Kimarekani nchini Ujerumani licha ya kuwaondoa wengine 5,000, na kambi muhimu za NATO zingali zimejikita nchini humo. Hata hivyo, utegemezi huo wa kijeshi hauwezi tena kufidia mvuto uliochujuka wa Marekani wa kiutamaduni na kiuchumi. Kizazi cha vijana wa Ujerumani kinahoji: “Kwa nini niende kusoma na kufanya kazi katika nchi ambayo hata raia wake waliohitimu masomo wameshindwa kupata ajira mwafaka?”
Matokeo ya kinachoendelea hivi sasa si mvutano wa kidiplomasia wa kupita tu. Ni tathmini ya uhalisia inayoakisi kuyoyoma kidogo kidogo kile kiitwacho "Ndoto ya Marekani" kwa mtazamo hata wa waitifaki na wakereketwa wa nchi hiyo.
Merz ameeleza bayana kwamba: "kwa sasa, usifiaji wangu hauongezeki".
Hii ni kauli ambayo raia wengi wa Ulaya wanakubaliana nayo ndani ya nyoyo zao. Marekani inabaki kuwa dola kubwa lenye nguvu, lakini sio tena mahali pasio na mshindani, kwa Wajerumani na watu wengine wa Ulaya wanaojenga mustakabali wao.../