Kuendelea hatua za mapinduzi za Marekani dhidi ya Venezuela
(last modified Sun, 10 Mar 2019 07:33:13 GMT )
Mar 10, 2019 07:33 UTC
  • Kuendelea hatua za mapinduzi za Marekani dhidi ya Venezuela

Uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela ungali unaendelea na katika hatua ya hivi karibuni kabisa, Washington imetishia kuziwekea vikwazo benki ambazo zinashirikiana na serikali ya Caracas.

Elliott Abrams, mjumbe maalumu wa serikali ya Marekani katika masuala ya Venezuela sanjari na kuashiria kwamba, Washington imo mbioni kupanua wigo wa vikwazo dhidi ya Venezuela amesema kuwa, Marekani inakusudia kuziwekea vikwazo zaidi taasisi za kifedha ambazo zinatekeleza amri za Nicolas Maduro.

Ni kwa muda sasa ambapo serikali ya Marekani imekuwa ikifanya njama za kutaka kuiangusha serikali ya mrengo wa kushoto ya Rais Nicolas Maduro na kuiweka madarakani serikali kibaraka.

Ikiwa na nia ya kufikia lengo hilo, hadi sasa Marekani imechukua hatua kadhaa kama kutilia shaka uchaguzi wa Rais nchini Venezuela, kutotambua duru ya pili ya uongozi wa Maduro, kutekeleza hatua za kuipindua serikali ya Caracas na kuwaunga mkono wapinzani wa Rais Maduro. Kwa hakika vikwazo ni wenzo mkuu wa Washington kwa ajili ya kuishinikiza serikali ya sasa nchini Venezuela.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela

Hadi sasa viongozi mbalimbali wa Venezuela, sekta ya mafuta, benki na kitengo cha mabadilishano ya fedha za kigeni zimekabiliwa na vikwazo.

Filihali, Marekani ikiwa na lengo la kupanua wigo wa mashinikizo dhidi ya serikali ya Venezuela imetishia kuziwekea vikwazo benki zinazoshirikiana na serikali ya Venezuela, hatua ambayo inakinzana wazi na sheria za kimataifa na hati ya Umoja wa Mataifa inayokataza kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. 

Ivan Timofeev, Mkurungezi wa Baraza la Mahusiano ya Kimataifa la Russia anasema kuwa: Marekani imekuwa ikijumuisha sheria zake za kitaifa kwa wageni, mashirika ya Ulaya, China, Russia na mtu mwingine yeyote. Kama benki na mashirika ya mataifa mengine yatakuwa na ushirikiano na shakhsia yeyote aliyewekewa vikwazo na Marekani, basi atajumuishwa katika vikwazo vya Washington. Vikwazo vya Marekani kwa mashirika makubwa ni hatari.

Marekani si tu kwamba, imeliweka katika ajenda zake suala la kupanua wigo wa vikwazo kwa ajili ya mashinikizo maradufu na kushadidisha matatizo ya kisiasa na kiuchumi nchini Venezuela, bali ikiwa na lengo la kuendeleza siasa zake za kutaka kuipindua serikali halali ya Rais Nicolas Maduro imekuwa ikiunga mkono hatua za uharibifu ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini, kama uharibifu uliofanywa dhidi ya Bwana la Guri la uzalishaji umeme, kituo kikubwa kabisa cha ugavi wa umeme nchini humo uliosababisha giza kwa siku kadhaa katika mji mkuu Caracas na mikoa mingine 15.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Kukatika umeme katika sehemu mbalimbali nchini Venezuela kuliibua wasiwasi wa kuchukua wigo mpana mgogoro wa nchi hiyo. Licha ya kuwa, wapinzani walifanya juhudi za kulinasibisha tatizo hilo na serikali na kwamba, sababu ya hilo ni uongozi mbaya na kutokuweko uwekezaji wa kutosha katika miundombinu vikiwmko vituo vya ugavi wa umeme, na hivyo kukoleza kuni katika moto wa mgogoro wa Venezuela, lakini viongozi wa serikali ya nchi hiyo wametangaza kuwa, hiyo ilikuwa hujuma ya mtandao.

Jorge Rodriguez, Waziri wa Mawasiliano wa Venezuela ametangaza kuwa, kukatika umeme nchini humo ilikuwa natija ya uharibifu na hujuma ya mtandao. Katika hujuma hiyo, mfumo wa kujiendesha wa kituo cha umeme cha Guri ulihujumiwa na kupelekea shughuli katika kituo hicho kukatika kwa muda. Kuna uwezekano hujuma hiyo ya uharibifu ilifanywa na Marekani.

Licha ya kuwa inaonekana kwamba, Marekani inatumia kila wenzo ilionao dhidi ya Venezuela kwa shabaha ya kuiondoa madarakani serikali ya Rais Maduro, lakini kiongozi huyo ameendelea kusimama kidete na kushinda njama zote kutokana na himaya na uungaji mkono wa jeshi na wananchi wa nchi hiyo.

Rais Mduro ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter:

Vita vya nishati ya umeme vilivyotangazwa na mabeberu wa Marekani dhidi ya wananchi wetu vitashindwa. Hakuna kitu wala mtu ambaye atawashinda wananchi wa Hugo Chavez (Rais wa zamani wa Venezuela).

Tags