Le Monde: Matajiri wa Marekani wanafadhili propaganda chafu dhidi ya Uislamu
Kundi dogo la matajiri na vibopa wa Marekani linafadhili mitandao inayosambaza habari na mashambulizi na propaganda chafu zinazoenezwa kupitia mtandao wa intaneti barani Ulaya kwa ajili ya kueneza fikra za mrengo wa kulia wenye misimamo mikali na kuchochea uadui dhidi ya Uislamu na matukufu yake.
Hayo yameripotiwa na gazeti mashuhuri la Le Monde nchini Ufaransa ambalo limeongeza kuwa, siyo nchi pekee zinazofanya propaganda chafu dhidi ya Uislamu katika vyombo vya habari bali kuna kundi dogo la matajiri na mabilionea wa Marekani wafadhili wa mrengo wa kulia ndani ya chama cha Republican wanaosaidia propraganda chafu na hujuma dhidi ya Uislamu kupitia njia ya kusambaza taarifa za uongo katika nchi nyingi za Ulaya.
Gazeti hilo limesema mabilionea hao wa Marekani wanaofadhili hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu hawana makundi mengi au majeshi katika mjitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter lakini wanatumia utajiri wao kufadhili makundi madogo madogo ya wanaharakati na mashirika ya mawasiliano yenye utaalamu kwa ajili ya kueneza fikra za makundi hayo.
Ripoti ya Le Monde imeongeza kuwa, Mkuregenzi Mtendaji wa kampuni ya Renaissance Technologies, Robert Mercer na binti yake, Rebeca ndio vinara wa kampeni hiyo ya matajiri wa Marekani ya kuchochea chuki dhidi ya Uislamu. Gazeti hilo limesema kuwa familia hiyo ya Mercer inafadhili mashirika na makampuni mengi yanayofanya propaganda chafu dhidi ya Uislamu kama kituo cha Horowitz na mtandao maarufu wa Breitbart News.
Hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu vimeongezeka sana katika nchi za Magharibi hususan baada ya Donald Trump kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani mwaka 2016.