EU yaionya Marekani isithubutu kuivamia kijeshi Venezuela
(last modified Wed, 13 Mar 2019 07:57:06 GMT )
Mar 13, 2019 07:57 UTC
  • EU yaionya Marekani isithubutu kuivamia kijeshi Venezuela

Umoja wa Ulaya umeionya Marekani kuhusu hatari ya chokochoko zake za kutaka kuivamia kijeshi Venezuela.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini aliyasema hayo jana Jumanne mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuonya kuwa, Marekani isijaribu kuivamia kijeshi Venezuela kwani matokeo ya uvamizi huo yatakuwa ni maafa makubwa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa EU ameongeza kuwa, Marekani inapaswa kuelewa kwamba kuna machaguo mengine bora zaidi kuliko hilo la kuivamia kijeshi Venezuela.

Amesema mgogoro wa Venezuela unaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia za amani, kama kupitia mazungumzo, diplomasia na mchakato wa kisiasa. 

Juan Guaidó (kushoto) na Mike Pence, Makamu wa Rais wa US

Licha ya Juan Guaidó kuungwa mkono na Marekani na nchi za Magharibi baada ya kujitangaza kuwa rais hapo tarehe 23 Januari mwaka huu, lakini hadi sasa hana nguvu yoyote nchini Venezuela kwa kuwa jeshi na vyombo vya mahakama vinamuunga mkono Rais Nicolás Maduro aliyechaguliwa kisheria. 

Itakumbukwa kuwa, Rais Nicolas Maduro alishinda uchaguzi wa rais uliofanyika kidemokrasia mwezi Mei mwaka jana nchini Venezuela na kuidhinishwa kutawala nchi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka 6.  

Tags