Mar 16, 2019 04:43 UTC
  •  Pompeo: Marekani itawanyima viza majaji wa mahakama ya ICC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa, nchi hiyo itawawekea marufuku ya viza ya kuingia Marekani maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai watakaotaka kuwasaili na kuwachunguza wanajeshi wa nchi hiyo wanaotuhumiwa kufanya jinai za kivita huko Afghanistan.

Tangazo la Mike Pompeo limetolewa baada ya serikali ya Marekani kutangaza mwezi Septemba mwaka jana kwamba, iwapo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai  (ICC) itaanzisha uchunguzi wa jinai za kivita huko Afghanistan itawapiga marufuku majaji na wendesha mashtaka wa mahakama hiyo kuingia Marekani, kuwawekea vikwazo vya fedha na kuwafungulia mashtaka katika mahakama za nchi hiyo.

Pompeo alisema jana Ijumaa kwamba, Marekani itawazuia kuingia nchini humo maafisa wa mahakama ya kimataifa ya ICC watakaohusika na kuwachunguza maafisa wa jeshi lake. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema marufuku hiyo ya viza pia yumkini ikatumiwa kuzuia jitihada za Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuwachunguza maafisa wa nchi waitifaki ikiwemo Israel.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadmu la Human Rights Watch, Andrea Prasow ametaja tangazo hilo la Mike Pompeo kuwa ni jaribio la kijambazi la kutaka kuwaadhibu wachunguzi wa vitendo vya kihalifu.

Askari wa Marekani wanatuhumiwa kufanya jinai dhidi ya binadamu Afghanistan

Prasow ameongeza kuwa: Kuwachukulia hatua maafisa wa mahakama ya kimataifa ya ICC kunatoa ujumbe kwa watesaji na wauaji kwamba jinai na uhalifu wao utaendelea bila ya kufuatiliwa. Vilevile amewataka wabunge wa Marekani kufuta hatua hiyo ya serikali ya Donald Trump na kuiunga mkono Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Novemba mwaka 2017 mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo aliomba idhini ya kuchunguza madai ya kufanyika jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu nchini Afghanistan tangu Mei Mosi mwaka 2003 yakiwemo maeneo ambako shirika la ujasusi la Marekani CIA linawashikilia watu katika jela za siri.   

Tags