Mikwaruzano inazidi kushadidi kati ya Marekani na Russia kuhusiana na Venezuela
(last modified Tue, 26 Mar 2019 06:54:25 GMT )
Mar 26, 2019 06:54 UTC
  • Mikwaruzano inazidi kushadidi kati ya Marekani na Russia kuhusiana na Venezuela

Kauli za tuhuma na uafriti wa Marekani dhidi ya Russia na Venezuela vimezidi kupamba moto kufuatia hatua ya Moscow kutuma shehena ya misaada nchini Venezuela.

Baada ya Russia kutuma ndege mbili zilizobeba shehena ya tani 35,000 za misaada zilizoandamana na askari wapatao 100 wa jeshi la nchi hiyo huko Venezuela, Marekani imesema, kuwepo kwa wanajeshi hao ni hatua ya kumlinda na kumhami rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo.

Katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo  ameituhumu Moscow kuwa "inaifanya hali ya mivutano inayoendelea nchini Venezuela iwe mbaya zaidi" na kueleza kwamba: "Washington na waitifaki wake katika Amerika ya Latini hawatakaa tu bila kuchukua hatua yoyote ya kukabiliana na Moscow."

Sergei Lavrov (kushoto) na Mike Pompeo 

Lavrov kwa upande wake hakuacha kujibu tuhuma hizo za Pompeo, ambapo katika taarifa maalumu aliyotoa baada ya mazungumzo ya simu aliyofanya na Pompeo, aliikosoa Marekani kwa "kula njama za kuratibu mapinduzi ya kijeshi nchini Venezuela."

Lavrov amebainisha katika taarifa yake hiyo kuwa, hatua kama hizo "zinakiuka Hati ya Umoja wa Mataifa na ni kisingizio cha kutaka kuingilia masuala ya ndani ya nchi iliyo huru na inayojitawala."

Tarehe 23 Januari, Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, akiungwa mkono wazi wazi na Marekani na waitifaki wake, alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela, hatua ambayo serikali na wananchi wa nchi hiyo waliitaja kuwa ni mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Nicolas Maduro na serikali yake halali iliyochaguliwa na wananchi waliowengi.../

Tags