Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amkejeli Bolton kwa kumshinikiza ajiuzulu
(last modified Sat, 30 Mar 2019 07:52:02 GMT )
Mar 30, 2019 07:52 UTC
  • Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amkejeli Bolton kwa kumshinikiza ajiuzulu

Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amemjibu Mshauri wa Rais katika Usalama wa Taifa wa Marekani, John Bolton aliyemtaka waziri huyo ajiuzulu.

Vladimir Padrino amejibu matamshi ya mara kwa mara ya Bolton ambaye amekuwa akimshinikiza waziri huyo na makamanda wa jeshi kujiuzulu na kuunga mkono kambi ya upinzani kwa kusema, "Bwana Bolton nikwambie tu kwamba sisi tunafanya jambo lililo sawa kwa kufuata na kuheshimu katiba. Kufanya kitu kilicho sawa ni kufuata yale yaliyoandikwa kwenye katiba na kutekeleza sauti ya wananchi."

Amebainisha kuwa, "Sisi ni askari wa kulinda ardhi zetu za asili, hatukubali kutwikwa rais katika kivuli cha maslahi ya nyuma ya pazia." 

Mwezi uliopita, licha ya kusema kuwa machaguo yote bado yako mezani, lakini Bolton alidai kuwa Washington inataka kufanyika mabadiliko ya utawala nchini Venezuela kwa njia ya amani, kauli ambayo ilionekana kuwa ya kulegeza msimamo Marekani, ambayo hapo awali ilisisitiza kuwa iko tayari kutumia njia ya kijeshi dhidi ya serikali halali ya Rais Nicolás Maduro.

Mshauri wa Rais katika Usalama wa Taifa wa Marekani, John Bolton 

Ikumbukwe kuwa mnamo Januari 23, kiongozi wa upinzani Juan Guaido alijitangaza kuwa rais wa Venezuela na punde baada ya hapo Marekani na baadhi ya madola ya Magharibi yalitangaza kumtambua.

Wananchi wa Venezuela na wanajeshi wa nchi hiyo pamoja na nchi nyingi na muhimu duniani kama vile Russia, China, Afrika Kusini, Iran na Uturuki zimepinga hatua hiyo sanjari na kutangaza kumuunga mkono kikamilifu Rais Maduro.

 

Tags