Iran yalaani jaribio la Marekani la kutaka kuipindua serikali ya Venezuela
(last modified Fri, 03 May 2019 03:57:42 GMT )
May 03, 2019 03:57 UTC
  • Iran yalaani jaribio la Marekani la kutaka kuipindua serikali ya Venezuela

Iran imelaani jaribio la hivi karibuni la Marekani la kutaka kuipindua serikali halali ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela.

Katika taarifa Alhamisi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Seyyed Abbas Mousavi ameionya Marekani kuhusu kuingilia mambo ya ndani ya Venezeula. Aidha amesema Iran inalaani jaribio lolote la kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya serikali ya Venezuela.

Tamko hilo limekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo na mwenzake wa ulinzi Patrick Shanahan pamoja na Mshauri wa Usalama wa Taifa Marekani John Bolton kutangaza kuunga mkono kikamilifu wapinzani waliohusika na jaribio la mapinduzi wakiongozwa na Juan Guaido.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kutishia kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya nchi nyingine ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Amebainisha masikitiko yake kuwa uthabiti wa kimatiafa unakabiliwa na tishio la wanasiasa wenye misimamo ya kufurutu ada na hivyo ni jukumu la jamii ya kimataifa kuchukua hatua kukabiliana na sera kama hizo.

Rais Maduro wa Venezuela

Mapema Jumanne Caracas, mji mkuu wa Venezuela ulishuhudia vurugu baada ya kundi dogo la wanajeshi kujiunga na Juan Guaido katika jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya mrengo wa kushoto inayoongozwa na Nicolas Maduro. Baada ya masaa machache Rais Maduro alihutubia taifa kwa njia ya televisheni na kutangaza kuwa jaribio hilo la mapinduzi limesabaratishwa.

Ikumbukwe kuwa, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais, Juan Guaido alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela hapo tarehe 23 Januari mwaka huu kupitia uungaji mkono kamili wa Marekani na washirika wa Washington. Hata hivyo licha ya njama hizo za kutaka kumuondoa madarakani Rais Maduro, jeshi na wananchi pamoja na nchi kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Afrika Kusini na mataifa mengi ya dunia yameendelea kusisitizia ulazima wa kuheshimiwa haki ya kujitawala nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

 

Tags