Usalama Waimarishwa misikitini Marekani kabla ya kuanza Mwezi wa Ramadhani
(last modified Mon, 06 May 2019 07:55:59 GMT )
May 06, 2019 07:55 UTC
  • Usalama Waimarishwa misikitini Marekani kabla ya kuanza Mwezi wa Ramadhani

Misikiti nchini Marekani imeimarisha usalama kwa kuwaajiri walinzi wenye silaha kabla ya kuanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Taarifa zinasema  kufuatia uzoefu mchungu wa kuhujumiwa misikiti katika eneo la Christchurch nchini New Zealand, misikiti mingi Marekani imewaajiri walinzi wenye silaha na pia kuweka makachero na kamera ili kuimarisha usalama.

Waislamu na wakuu wa miji kadhaa Marekani wamebainisha wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa kutekelezwa hujuma kama zile zilizolenga misikiti miwili  nchini New Zealand.

Ikumbukwe kuwa  Machi 15 misikiti miwili ya Noor na Linwood katika mji wa Christchurch New Zealand ilihujumiwa na gaidi wakati wa Sala ya Ijumaa ambapo Waislamu wasiopungua 51 waliuawa shahidi.

Msikiti wa Christchurch New Zealand

Mtekelezaji wa hujuma hiyo ya kigaidi ni raia wa Austrilia mwenye umri wa miaka 28 ambaye katika kurasa zake za kijamii alikuwa ametuma taarifa za kibaguzi na kulaani kuwepo Waislamu katika nchi za Magharibi. Aidha gaidi huyo alijitangaza kuwa mfuasi sugu wa Rais Trump wa Marekani.

Baada ya ugaidi huo wa New Zealand,  kumeenea hofu miongoni mwa Waislamu Marekani hasa baada ya misikiti kupokea vitisho.

Tokea Trump aingie madarakani na baada ya makundi ya wabaguzi wa rangi kuunga mkono misimamo yake ya kichochezi, kumesuhudiwa ongezeko la hujuma dhidi ya Waislamu na vituo vya Kiislamu nchini Marekani