China na Russia kususia mkutano wa Marekani dhidi ya Palestina, Bahrain
Serikali za China na Russia zimetangaza kuwa hazitashiriki mkutano wa Marekani wa kuzindua hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa 'Muamala wa Karne' mwezi ujao wa Juni nchini Bahrain.
Balozi wa China huko Palestina, Guo Wei amemuambia Nabil Shaath, mshauri wa masuala ya kigeni wa Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuwa, Beijing na Moscow zimeafikiana juu ya kuususia mkutano huo.
Shirika la habari la Palestina la Wafa limemnukuu balozi huyo ambaye amesema kuwa, "Kulisusia Kongamano la Bahrain ni katika fremu ya mkataba wa maelewano uliosaniwa kati ya Beijing na Moscow ambazo zimekubaliana kutoshiriki."
Wei amesisitiza kuwa, sera ya Beijing ni kuunga mkono kadhia ya Palestina ikiwemo haki ya kuundwa taifa huru la Palestina kwa mujibu wa mipaka ya 1967, mji mkuu wake ukiwa Quds.
Wapalestina wamekuwa wakiulaani na kuupinga vikali mpango huo wa 'Muamala wa Karne' wakiutaja kuwa ni moja ya njama kubwa zaidi dhidi ya taifa madhulumu la Palestina linalokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel.
Mkwe wa Rais Donald Trump wa Marekani, Jared Kushner hivi karibuni alifichua kuwa, hatua ya kwanza ya 'Muamala wa Karne' itazinduliwa na Marekani nchini Bahrain katika 'Kongamano la Kiuchumi' litakalofanyika Juni 25 na 26.