Marekani yakiri kutumia Intaneti kushambulia nchi nyingine
Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani ametangaza waziwazi kuwa Washington inatumia mawasiliano ya kumpyuta kushambulia baadhi ya nchi duniani.
Shirika la habari la Sputnik limemnukuu John Bolton akisema hayo jana Jumanne na kuongeza kuwa, Marekani inaendesha mashambulizi ya mawasiliano ya kompyuta dhidi ya Russia na baadhi ya nchi ili kuzionesha madhara ya kuingilia masuala ya ndani ya Marekani.
Kukiri huko kwa Bolton kumekuja katika hali ambayo hadi hivi sasa Marekani imeziwekea nchi kadhaa vikwazo kwa madai ya kufanya mashambulizi ya mawasiliano ya kompyuta dhidi ya Washington.
Mara kadhaa Marekani na waitifaki wake wamekuwa wakiituhumu Russia kuwa inaendelesha mashambulizi ya mawasiliano ya kompyuta dhidi ya nchi hizo.
Mara zote Russia imekuwa ikikanusha madai hayo na kutaka ushirikiano wa kimataifa wa kulindwa usalama wa mawasiliano ya kompyuta.
Washington inaituhumu pia Russia kuwa iliingilia na kuchakachua matokeo ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 huko Marekani na kuyafanya matokeo hayo yaoneshe kuwa Donald Trump ndiye aliyeshinda uchaguzi huo, madai ambayo yanaendelea kukanushwa vikali na Moscow.