Rais Rouhani asisitiza kuimarishwa uhusiano wa Iran na Afghanistan
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran inataka kuona uthabiti, usalama, amani na utulivu katika nchi jirani ya Afghanistan huku akisisitiza umuhimu wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili.
Rais Hassan Rouhani ameyasema hayo leo Jumamosi asubuhi mjini Doushanbe nchini Tajikistan alipokutana na Abdullah Abdullah, Mtendaji Mkuu katika serikali ya Afghanistan pembizoni mwa Mkutano wa Tano wa Kongamano la Maingiliano na Hatua za Kujenga Imani Barani Asia (CICA). Rais Rouhani ameongeza kuwa, kuna uwezo mkubwa wa kuimarishwa uhusiano wa kiuchumi wa nchi mbili na kieneo hasa usafirishaji bidhaa na hivyo kamisheni za ushirikiano wa pande mbili zinapaswa kukutana kujadili maudhui hiyo.
Rais wa Iran pia ameashiria umuhimu wa kupambana na dawa za kulevya na kuongeza kuwa: "Mbali na matatizo ya kijamii, biashara haramu ya dawa za kulevya pia kufadhili ugaidi kifedha."
Rais wa Iran pia amesema kushirikishwa Waafghani wa makundi na kaumu zote katika kuleta uthabiti nchini humo ni jambo la dharura. Aidha ametaka sekta binafsi zishajiishwe katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara wa nchi mbili.
Kwa upande wake. Abdullah Abdullah, Mtendaji Mkuu katika serikali ya Afghanistan ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa himaya na misaada yake kwa watu wa Afghanistan huku akisisitiza kuhusu kuimarishwa ushirikiano wa nchi mbili katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kibiasahra.
Abdullah Abdullah pia ameipongeza Iran kwa jitihada zake za kukabiliana na mihadarati na kusema kuna udharura wa ushurikiano zaidi baina ya Tehran na Kabul katika uwanja huo.