Russia: Marekani inapaswa kurejea haraka kwenye JCPOA
Russia imesema Marekani inapaswa kurejea mara moja kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.
Sergey Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Washington inapaswa kurejea haraka iwezekanavyo kwenye makubaliano hayo, sanjari na kutekeleza wajibu wake kwenye mapatano hayo kwa mujibu Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Amesema hatua za kujibu mapigo zinazochukuliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran licha ya kuwa zipo ndani ya vipengee vya makubaliano hayo, lakini zimechochewa na mashinikizo kutoka pande ambazo hazifungamani na mapatano hayo ya kimataifa.
Kutokana na hali hiyo ya kulegalega nchi za Ulaya katika utekelezaji wa mfumo huo, Rais Hassan Rouhani wa Iran tarehe 8 mwezi uliopita alisema kwamba Tehran imesitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kukiwemo kuongeza akiba ya urani yake iliyorutubishwa pamoja na maji mazito ya nyuklia.
Alisisitiza kwamba kama katika kipindi cha siku 60 nchi za Ulaya zitashindwa kuchukua hatua za kukabiliana na vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran, basi Tehran itachukua hatua zaidi.
Kwa sasa inafanya mazungumzo na nchi za Ulaya kwa ajili ya kujiunga na mfumo maalumu wa mabadilishano ya kibiashara baina ya Ulaya na Iran (INSTEX), ambao ulikamilishwa mwezi Februari mwaka huu lakini hadi sasa bado haujaanza kutekelezwa.