Serikali ya Marekani yajiandaa kuwatimua wahajiri ambao hawajasajiliwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i54701-serikali_ya_marekani_yajiandaa_kuwatimua_wahajiri_ambao_hawajasajiliwa
Serikali ya Marekani imeamua kuanzia wiki ijayo kutekeleza operesheni kubwa ya msako wa kuwakamata na kuwafukuza nchini humo wahajiri ambao hawajasajiliwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 11, 2019 21:54 UTC
  • Serikali ya Marekani yajiandaa kuwatimua wahajiri ambao hawajasajiliwa

Serikali ya Marekani imeamua kuanzia wiki ijayo kutekeleza operesheni kubwa ya msako wa kuwakamata na kuwafukuza nchini humo wahajiri ambao hawajasajiliwa.

Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, baada ya kumalizika muhula wa wiki mbili uliotolewa na rais wa nchi hiyo Donald Trump, kuanzia siku ya Jumapili ijayo, maafisa wa Idara ya Utendaji ya Forodha na Uhajiri, wataanzisha operesheni kubwa ya msako wa kuwakamata na kuwahamisha nchini humo wahajiri wapatao elfu mbili ambao hawajasajiliwa; msako ambao utafanywa katika miji mikubwa kumi ya nchi hiyo.

Kulingana na tamko lililotolewa na maafisa wa Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani, operesheni hiyo ambayo imepangwa kutekelezwa kwa muda wa siku kadhaa, itajumuisha hata wahajiri waliopata kibali cha kuishi nchini humo kwa dhamana.

Askari wa Marekani akimpekua mtu anayeshukiwa kuwa mhajiri haramu

Tangu wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 na baada ya kuingia madarakani pia, kupambana na wahajiri ambao hawajasajiliwa, imekuwa moja ya ajenda kuu inayopigiwa upatu na Trump, ambapo hadi sasa rais huyo wa Marekani ameshachukua hatua kadhaa ikiwemo ya kujenga uzio kwenye mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Mexico na kutuma vikosi vya jeshi katika eneo hilo.

Sera za kupiga vita wahajiri za Trump zimekuwa zikikosolewa vikali ndani na nje ya Marekani.../