Maelfu waandamana Marekani kupinga udhalilishaji wa Trump kwa wahajiri
Maelfu ya watu wamefanya maandamano katika miji mbalimbali ya Marekani, kupinga sera hasi za utawala wa Rais Donald Trump dhidi ya wahajiri wanaozuiliwa katika vituo vya mpaka wa nchi hiyo, na pia dhidi ya mpango wa kuwakamata na kuwatimua nchi humo wahajiri ambao hawajasajiliwa.
Katika mji mkuu Washington, waandamanaji hao jana Ijumaa walikusanyika nje ya Ikulu ya White House, ambapo walisikika wakipiga nara dhidi ya sera za udhalilishaji za Trump dhidi ya wahajiri.
Baadhi ya waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango yaliyokuwa na jumbe zinazosema: "funga jela za wahajiri", "waachie huru watoto wahajiri" na "utumwa mambo leo".
Utawala wa Trump kuanzia kesho Jumapili unatazamiwa kuanza kutekeleza operesheni kubwa ya kuwakamata na kuwafukuza nchini humo wahajiri wapatao elfu mbili ambao hawajasajiliwa katika miji mikubwa kumi ya nchi hiyo.
Wiki iliyopita, Michelle Bachelet Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa sanjari na kukosoa vikali sera za wahajiri za utawala wa Trump, alieleza kusikitishwa kwake na hali mbaya inayowakabili wahajiri na wakimbizi nchini Marekani.
Hivi kariuni, Rais Donald Trump alitoa kauli ya kejeli na dharau dhidi ya wahajiri nchini humo na kusema kuwa: "Kama hali ni mbaya katika vituo vya wahajiri mpakani, basi wahajiri hao waambiwe wasije nchini hapa. Wenyewe wamekimbia umaskini wa kupindukia katika nchi zao."