Nyaraka za CIA zinazohusiana na mauaji ya Khashoggi zafichuliwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i55452-nyaraka_za_cia_zinazohusiana_na_mauaji_ya_khashoggi_zafichuliwa
Shirika la ujasusi la Marekani CIA limefichua baadhi ya nyaraka zinazohusiana na mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 18, 2019 08:52 UTC
  • Nyaraka za CIA zinazohusiana na mauaji ya Khashoggi zafichuliwa

Shirika la ujasusi la Marekani CIA limefichua baadhi ya nyaraka zinazohusiana na mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi.

Shirika la ujasusi la Marekani limetoa nyaraka hizo za mauaji ya Khashoggi baada ya mashtaka yaliyowasilishwa na taasisi moja ya sheria na hukumu iliyotolewa na mahakama ya kikanda ya Marekani.

Sehemu moja ya nyaraka hizo imeashiria nafasi ya mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman katika mauaji ya Jamal Khashoggi na kusema kuwa uchunguzi wa wataalamu wa CIA unaonesha kuwa, Bin Salman alihusina katika mauaji hayo.

Nyaraka hizo za CIA pia zinafichua barua na ujumbe zilizokuwa zikiandikwa baina ya maajenti wa CIA kuanzia tarehe 16 Novemba 2018 yaani wiki moja tu baada ya mauaji ya Jamal Khashoggi. 

Nyaraka hizo zimetolewa baada ya Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la CIA Jenna Haspel kuliambia Baraza la Seneti la Marekani Disemba mwaka jana kwamba mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia, Muhammad bin Salman ndiye aliyeamuru mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi. Jenna Haspel aliongeza kuwa mauaji ya kutisha ya mwandishi huyo ndani ya ubalozi wa Saudia mjinI Istanbul yalifanyika kwa amri ya Bin Salman na kwamba kuna watu katika serikali ya Trump wanataka kuficha kadhia hiyo. 

Jamal Khashoggi ambaye aliwahi kuwa mtu wa karibu sana kwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia lakini baadaye akageuka na kuwa mkosoaji mkubwa wa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo Muhammed bin Salman, aliuawa kikatili akiwa ndani ya ubalozi wa Saudia mjini Istanbul na mwili wake ukakatwa vipande vipande na kupelekwa kusiko julikana. Mauaji hayo yalifanywa na timu ya maafisa usalama wa Saudi Arabia.