Alkhamisi, tarehe 05 Februari, 2026
Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Sha'bani 1447 Hijria, sawa na Februari 5 mwaka 2026.
Katika siku kama ya leo miaka 145 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle.
Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 katika familia ya watu wa kijijini na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu na baadaye alianza kufunza lugha hiyo katika Chuo Kikuu cha Cambridge,London. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo.
Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo."
Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha na kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza. ****
Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilikiri kushindwa kutabiri masuala ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Maafisa wa CIA walikiri kuwa shirika hhilo limeshindwa kutabiri matukio ya Iran. Walisema, kitu ambacho hatukukitabiri kabisa ni mtu mmoja mzee wa miaka 78 ambaye alibaidishwa nje ya nchi kwa muda wa miaka 14, kuweza kuwaunganisha kiasi chote hiki wananchi wa Iran. ***
Miaka 28 iliyopita katika siku hii, yaani tarehe 16 Bahman 1376 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Hujjatul Islam "Jalil Honaravar Khoei."
Jalil Honaravar Khoei alizaliwa mwaka 1305 Hijria Shamsia yaani mwaka 1345 Hijria Qamaria katika mji wa Khoei wa mkoa wa Azarbaijan Magharibi nchini Iran. Alianza mapema kusoma masomo ya dini. Katika miaka kumi na minne ya umri wake, alijifunza fasihi na usul na kutabahari katika fani hizo.
Kuanzia mwaka 1337 Hijria Shamsia, alichukua jukumu la kusimamia chuo muhimu cha kidini cha mji huo kwa muda wa miaka 20. Katika kipindi hiki na hadi mwisho wa maisha yake, alifundisha sayansi ya dini na kufunza makumi ya masheikh na walimu mahiri waliondeleza juhudi zake baada yake. Alikuwa akitumia siku nzima kuanzia asubuhi hadi jioni kufundisha mafundisho ya Ahlul-Bayt AS.
Alikuwa akitumia muda wake mwingine kutatua masuala ya watu, kuhudumia Waislamu, kutatua hitilafu zao, kujibu maswali yao ya kidini, kusimamia misikiti na shule, na alikuwa akisoma vitabu mbalimbali katika wakati wake wa faragha. Alikuwa na umahiri mkubwa wa Tafsir ya Qur’ani, tarikhi, hadithi na fasihi ya Kiarabu na Kiajemi na ameirithisha vizazi vya baada yake turathi yenye thamani kubwa.
Miongoni mwa athari za thamani za Hujjatul Islam Jalil Honaravar Khoei ni kitabu cha "Ufafanuzi wa Majina" ambacho kimehifadhi maelezo ya majina ya Mitume na Manabii, Maimamu, na wanazuoni wa Kishia na Kisuni. ***
Katika siku kama ya leo miaka mitatu iliyopita Pervez Musharraf, Rais wa kumi wa Pakistan, alifariki dunia.
Musharraf alizaliwa mnamo Agosti 11, 1943, huko Naharwali Haveli, katika wilaya ya Daryaganj karibu na Delhi, katika India iliyokuwa ikitawaliwa na Uingereza. Baada ya kugawanywa India, alihamia Pakistan na wazazi wake na kuishi Karachi. Aliingia Chuo cha Kijeshi cha Pakistani huko Kakul mnamo 1961 na baada ya kuhitimu, alijiunga na jeshi na akapanda safu za juu za uuongozi.
Mwaka 1998, Pervez Musharraf aliteuliwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu na Waziri Mkuu Nawaz Sharif, na Oktoba 12, 1999, akawa kiongozi wa serikali ya Pakistani baada ya kumwondoa madarakani Nawaz Sharif katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu.
Musharraf alikuwa jenerali wa nne wa Pakistan kutawala nchi hiyo kwa miaka tisa kupitia njia ya mapinduzi. Hatimaye alitangaza kujiuzulu wadhifa wake wa urais katika hotuba yake kwa njia ya televisheni mnamo Agosti 18, 2008, baada ya mirengo ya upinzani katika Bunge la Pakistan kutia kumfungulia mashtaka na kumuondoa madarakani.
Musharraf aliaga dunia tarehe 5 Februari 2023, katika hospitali huko Dubai akiwa na umri wa miaka 79 baada ya kustahamili ugonjwa kwa muda mrefu. ****