Venezuela: Tutaichukulia hatua Colombia katika Umoja wa Mataifa
(last modified Mon, 02 Sep 2019 04:06:14 GMT )
Sep 02, 2019 04:06 UTC
  • Venezuela: Tutaichukulia hatua Colombia katika Umoja wa Mataifa

Serikali ya Venezuela imesema kuwa itawasilisha ushahidi kwa Umoja wa Mataifa kuhusu misaada na uungaji mkono unaotolewa na Colombia kwa makundi yanayobeba silaha ya upinzani dhidi ya serikali ya Rais Maduro.

Bi Delcy Rodriguez Makamu wa Rais wa Venezuela ameeleza kuwa nchi yake ina ushahidi wa wazi kuhusu uungaji mkono wa Rais Ivan Duque wa Colombia kwa makundi ya kigaidi na kutoa mafunzo na kuyapatia silaha makundi hayo.  Amesema Venezuela itakabidhi ushahidi huo kwa Umoja wa Mataifa. 

Makamu wa Rais wa Venezuela amesema, hatua hizo za Colombia zinakiuka azimio nambari 1373 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo ambalo lilipasishwa Septemba 28 mwaka 2001 ni waraka wa kimataifa kuhusu vitisho vya amani na usalama wa kimataifa vinavyotokana na vitendo vya utumiaji silaha. 

Juzi Jumamosi  Jorge Rodriguez Waziri wa Mawasiliano na Habari wa Venezuela pia alitangaza kuwa kuna kambi nchini Colombia ambayo inafanya kazi ya kuwapa mafunzo wanamgambo ili kujiandaa kutekeleza mashambulizi dhidi ya serikali ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela. Serikali ya Colombia inashirikiana na Marekani kuipinga serikali halali ya Venezuela huku zikimuunga mkono Juan Guaido kiongozi wa upinzani nchini humo. 

Rais halali wa Venezuela, Nicolas Maduro
 

 

 

Tags