Maombolezo ya Ashura ya Imam Hussein AS yaadhimishwa kote duniani
(last modified Tue, 10 Sep 2019 03:37:36 GMT )
Sep 10, 2019 03:37 UTC
  • Maombolezo ya Ashura ya Imam Hussein AS yaadhimishwa kote duniani

Mamilioni ya Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maeneo mengine ya dunia hii leo wanaadhimisha siku ya Ashura ya kukumbuka alipouawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS.

Imam Husain AS aliuawa shahidi kikatili na kinyama mwaka wa 61 Hijria katika jangwa la Karbala nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 57 baada ya kuongoza mapambano ya kishujaa ya ushindi wa damu mbele ya upanga.

Mtume Muhammad SAW alitabiriwa na Malaika Jibril ukatili huo aliofanyiwa mjukuu wake katika jangwa la Karbala, tangu enzi za uhai wake na alikuwa wa kwanza kumlilia mjukuu wake huyo kipenzi baada ya kuletewa mchanga na Malaika Jibril, wa eneo ambalo Imam Hussein AS angeliuliwa shahidi.

Moja ya vikao vya maombolezo ya Ashura nchini Iran

Kwa kufuata sira na mwenendo huo wa Bwana Mtume Muhammad SAW, wafuasi wa Ahlul Bayt wa Mtume na wapenzi wa haki na wanaopiga vita dhulma, wanaendelea hadi leo hii katika kila kona ya dunia, kukumbuka kwa huzuni na majonzi jinai hiyo kubwa waliyofanyiwa watu wa nyumba tukufu ya Bwana Mtume Muhammad SAW na kumbukumbu hizo huwa kubwa zaidi katika siku kama ya leo ya mwezi kumi Muharram kila mwaka.

Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote na kwa kila mpenda haki na ukombozi duniani kwa mnasaba wa kukumbuka msiba huu mkubwa uliomfika Bwana Mtume Muhammad SAW na Uislamu kiujumla.