Ujerumani yarefusha kwa miezi sita mingine marufuku ya silaha kwa Saudia
Serikali ya Angela Merkel imeongeza kwa miezi mingine sita marufuku ya silaha zote za Ujerumani inazoziuzia Saudi Arabia licha ya miito inayotaka kulegezwa marufuku hiyo.
Serikali ya Ujerumani imesema kuwa marufuku hiyo imerefushwa kwa miezi sita hadi Machi 31 2020 ambapo itatazamwa upya kwa mara nyingine tena. Marufuku hiyo ya Ujerumani ya kuiuzia silaha Saudia iliwekwa kwa mara ya kwanza mwaka juzi 2017 kwa sababu za kibinadamu kutokana na vita huko Yemen; na kisha marufuku hiyo ikaimarishwa mwaka jana kufuatia mauaji ya mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Aal Saud, Jamal Khashoggi ambaye aliuliwa kinyama katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul Uturuki Oktoba mwaka jana.
Mbunge mwenye ushawishi katika chama cha Kansela Angela Merkel jana alipendekeza kulegezwa marufuku hiyo ya silaha ili kuruhusu kuiuzia Saudia silaha eti za kujilinda hata hivyo Angela Merkel alisema kuwa haoni hatua wala mazingira yoyote yanayoweza kubadili msimamo wa Ujerumani katika uwanja huo. Saudi Arabia na waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati wanaendesha vita dhidi ya watu wa Yemen tangu Machi 2015 kwa kutumia silaha na zana zingine za kijeshi kutoka nchi za Magharibi khususan Marekani, Ufaransa, Uingereza na Canada.
Marufuku hiyo ya Ujerumani ya kuiuzia Saudi Arabia silaha hata hivyo imepongezwa na watetezi wa haki za binadamu ambao wamesema kuwa imekuwa na taathira kubwa kuliko ilivyotarajiwa.