Kuvunjika mzungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Korea Kaskazini
(last modified Mon, 07 Oct 2019 09:59:13 GMT )
Oct 07, 2019 09:59 UTC
  • Kuvunjika mzungumzo ya nyuklia kati ya Marekani na Korea Kaskazini

Rais wa Marekani Donald Trump wa Marekani, anaendelea na siasa za vitisho na mazungumzo katika fremu ya ahadi zake za uchaguzi za kuutatua mgogoro wa nyuklia wa Rasi ya Korea.

Hata hivyo na licha ya kufanyika duru tatu za mazungumzo kati ya viongozi wa Korea Kaskazini na Marekani, hadi sasa hakujapatikana maendeleo ya kweli ya kuweza kutatua mgogoro wa eneo hilo. Kwa kuzingatia mashinikizo ya serikali ya Marekani kwa ajili ya kuanza duru mpya ya mazungumzo baina ya Washington na Pyongyang, na ikiwa ni baada ya kupita miezi kadhaa ya kusimama mazungumzo ya pande mbili, Jumamosi ya tarehe tano mwezi huu, jumbe za Marekani na Korea Kaskazini zilifanya mazungumzo mjini Stockholm, Sweden, ingawa hata hivyo mazungumzo hayo yalikwama baada ya kupita saa chache tangu yaanze. Kim Myong-Gil, kiongozi wa ujumbe wa wataalamu wa Korea Kaskazini ameelezea sababu zilizopelekea kukwama mazungumzo hayo kwa kusema: "Mazungumzo haya hayakidhi matarajio ya nchi. Marekani haijaleta kitu chochote kipya na badala yake inasisitizia tu kutekelezewa matakwa yake ya huko nyuma." Kwa kweli ni Washington ndiyo iliyofanya njama za kukwamisha mazungumzo hayo. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na katika radiamali yake kuhusiana na matamshi ya kiongozi wa timu ya mazungumzo ya Korea Kaskazini, imedai kuwa, matamshi hayo yanatofautiana na 'hali ya mambo inayotawala' juu ya mazungumzo hayo. Kadhalika wizara hiyo ya mambo ya nje ya Marekani imedai kuwa, mazungumzo kati ya pande mbili yalidumu kwa muda wa masaa sita na yalikuwa na natija nzuri. 

Viongozi wa timu za mazungumzo wa nchi mbili huko Sweden

Morgan Ortagus, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amedai kuwa, "Washington iliwasilisha mapendekezo ya kiubunifu, hata hivyo ili kufikiwa njia ya utatuzi wa masuala umuhimu, pande zote mbili ni lazima ziwe na azma ya dhati." Licha ya kwamba kiongozi wa timu ya mazungumzo ya Korea Kaskazini ameelezea kuvunjika na kutokuwa na natija yoyote mazungumzo hayo, lakini upande wa Marekani umetangaza kwamba pande mbili zimekubaliana na pendekezo la Sweden la kuendelezwa mazungumzo katika kipindi cha wiki mbili zijazo. Mazungumzo ya wataalamu kutoka Washington na Pyongyang huko mjini Stockholm, Sweden, ni duru ya kwanza ya mazungumzo ya pande mbili tangu Donald Trump na Kim Jong-un walipokutana mwezi Februari huko Hanoi, mji mkuu wa Vietnam, mazungumzo ambayo hata hivyo yalimalizika bila kufikiwa natija na hata kabla ya muda wake uliopangwa awali. Katika mazungumzo hayo, viongozi wa nchi hizo mbili walishindwa kufikia natija kuhusiana na masuala muhimu, yaani suala la kuangamizwa silaha za nyuklia katika eneo la Korea. Hii ni kusema kuwa baada ya Marekani kuwasilisha mapendekezo yasiyo ya kimatiki, iliitaka serikali ya Korea Kaskazini kuangamiza kikamilifu silaha zake za nyuklia, tena bila ya Washington kuupatia upande wa pili haki ya kuwasilisha mapendekezo yake, yaani ya kuondolewa vikwazo ambavyo imewekewa serikali ya Pyongyang. Hiyo ndiyo sababu hasa iliyopelekea kuvunjika mazungumzo hayo, huku Korea Kaskazini ikianzisha majaribio ya makombora yake ya balestiki. Pamoja na hayo Trump na Kim Jong-un walikutana tena mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu katika mpaka wa Korea mbili, ambapo walikubaliana kuendelezwa mazungumzo ya nchi mbili kwa ngazi ya wataalamu.

Trump, mtu muongo asiyeaminiwa katika mazuungumzo

Kwa mara kadhaa Pyongyang imekuwa ikiishutumu serikali ya Washington kuwa inaendeleza mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Korea Kaskazini, licha ya nchi hiyo kutekeleza kwa upande mmoja baadhi ya matakwa ya Marekani. Kwa kuzingatia kuwa Kim Jong-un, Kiongozi wa Korea Kaskazini anafahamu vyema namna ya kucheza karata zake mbele ya Marekani, yaani anafahamu namna ya kuinua uwezo wa silaha za nyuklia na uwezo wa makombora ya balestiki ya nchi yake, hivyo hayupo tayari hata kidogo kupunguza uwezo wa kijeshi ya nchi yake kabla ya upande wa pili kuipatia Pyongyang nafasi ya kutekelezewa matakwa yake yaani ya kuondolewa vikwazo na Washington. Hii ni kusema kuwa, Marekani inaitaka Korea Kaskazini mbali na kuachana na silaha zake za nyuklia, pia iiwekee mipaka miradi yake ya makombora. Mkabala wa mapendekezo hayo, serikali ya Pyongyang imetangaza kuwa ili ikubaliane na matakwa hayo ya Marekani, ni sharti kwanza kuchukuliwe hatua za kivitendo za kuondolewa vikwazo dhidi yake japo hatua kwa hatua. Hata hivyo kwa kuzingatia mashinikizo makali ya ndani dhidi ya Donald Trump hususan suala la kusailiwa na uwezekano wa kupokonywa urais, rais huyo wa Marekani anafanya juhudi za kila namna za kuonyesha amepata mafanikio nje ya Marekani ili kupunguza mashinikizo ya ndani. Hata hivyo kitendo chake cha kukwamisha mazungumzo ya Stockholm kati yake na Korea Kaskazini, kinaonesha kuwa Washington inataka kupata mafanikio hayo bila ya gharama yoyote. Hivyo, hata kama tutayasadiki madai ya ujumbe wa Marekani ya kufanyika mazungumzo mengine wiki mbili zijazo, lakini bado tunaweza kusema kuwa mazungumzo hayo nayo hayatokuwa na matunda yoyote.

Tags