Putin: Nchi za Kiarabu ziheshimu Iran na maslahi yake katika eneo
(last modified Sun, 13 Oct 2019 08:09:54 GMT )
Oct 13, 2019 08:09 UTC
  • Putin: Nchi za Kiarabu ziheshimu Iran na maslahi yake katika eneo

Rais Vladimir Putin wa Russia ameziasa nchi za Kiarabu na nyinginezo katika Ghuba ya Uajemi na eneo la Asia Magharibi kuiheshimu Iran na kuitambua kama taifa lenye uwezo mkubwa katika eneo.

Putin amesema hayo katika mahojiano na kanali tatu mashuhuri za televisheni zinazorusha matangazo yao kwa lugha ya Kiarabu na kusisitiza kuwa, nchi za eneo zinapaswa kuheshimu haki na maslahi ya Iran na kuitazama kama taifa kubwa lenye historia kongwe katika eneo.

Rais wa Russia amebainisha kuwa, wakati umefika kwa majirani za Iran kutambua kuwa taifa hilo limekuwepo kwa maelfu ya miaka na ukweli huo hauwezi kufutika.

Rais Vladimir Putin amesisitiza kuwa Russia inataka kuwa na uhusiano na ushirikiano wa karibu na Iran na nchi za eneo la Asia Magharibi licha ya taharuki iliyopo.

Meli ya mafuta ya Iran iliyoshambuliwa karibu na pwani ya Saudia

Kuhusu kushambuliwa meli ya mafuta ya Iran katika maji ya kimataifa, Putin amesema kushambuliwa meli za mafuta katika maji ya kieneo ni jambo ambalo linapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote kwa kuwa vitendo hivyo vinaweka hatarini usalama wa nishati duniani.

Kadhalika amegusia operesheni ya Uturuki huko kaskazini mwa Syria na kubainisha kuwa, "Syria inapaswa kuwa huru kutokana na vikosi ajinabi. Vikosi vamizi katika taifa lolote la eneo vinapaswa kuondoka mara moja. Hata sisi tupo tayari kuondoka Syria iwapo serikali ya Damascus itasema haihitajii tena msaada wetu."