Katibu Mkuu wa UN azitaka serikali zishughulikie matakwa ya wananchi wao
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuachwa vitendo vya utumiaji mabavu na machafuko katika mikusanyiko na maandamano, na kuzitaka serikali ziyashughulikie matatizo halisi waliyonayo wananachi wao.
Antonio Guterres ametoa mwito huo mbele ya waandishi wa habari katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na akaongezea kwa kusema: Tunashuhudia wimbi la maandamano duniani kote, kuanzia Magharibi ya Asia, Amerika ya Latini mpaka Carribean na kuanzia Ulaya, Afrika hadi Asia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, baadhi ya maandamano yanatokana na matakwa ya kisiasa, na katika baadhi ya maandamano, wananchi wanalalamikia ongezeko la bei za bidhaa, ufisadi na aina mbali mbali za ubaguzi na upendeleo.
Huku akisisitiza kwamba kuna masuala kadhaa ya pamoja katika maandamano yote ya upinzani, hivyo inapasa yazingatiwe, Guterres amesema: "Imani kati ya wananchi na mifumo ya kisiasa imepungua."
Kwa mujibu wa Guterres, dunia imeathiriwa pia na taathira za utandawazi pamoja na teknolojia mpya, ambazo zimesababisha kuongezeka utovu wa usawa katika jamii za watu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonyesha kutiwa wasiwasi pia na hali ya kisiasa ya Iraq na maandamano ya upinzani yanayofanywa na wananchi nchini humo.
Siku ya Alkhamisi iliyopita, sambamba na kuanza maandamano ya usiku ya wananchi, Waziri Mkuu wa Iraq Adil Abdul-Mahdi alitangaza mageuzi kadhaa ya kisiasa serikalini.
Huku akisisitiza kwamba serikali inaunga mkono maandamano ya amani, Waziri Mkuu wa Iraq amebainisha kuwa, mnamo wiki ijayo yatafanyika mageuzi kadhaa katika wizara za serikali.../