UN: Watoto milioni 7 wapo kizuizini, Marekani yaongoza
Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa, watoto zaidi ya milioni saba wanashikiliwa katika jela na vituo mbalimbali duniani, huku Marekani ikiongoza katika orodha hiyo.
Kwa mujibu wa Manfred Nowak, mkuu wa utafiti uliofanywa na UN, kati ya watoto laki tatu wahajiri waliopo kizuizini katika maeneo mbalimbali duniani, laki moja wapo katika jela na vituo vya mpakani vya kuwazuilia wahajiri nchini Marekani.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, akthari ya watoto hao ni wale waliotenganishwa na wazazi wao na wanakabiliwa na matatizo ya kimwili na kisaikolojia.
Takwimu zilizotolewa na serikali ya Marekani hivi karibuni hata hivyo zinaonyesha kuwa, idadi ya watoto wahajiri wanaoshikiliwa jela mwaka huu wa 2019 inakaribia elfu 70 na kwamba kiwango hicho kimeongezeka kwa asilimia 42 kikilinganishwa na cha mwaka jana.
Ripoti zinasema kuwa, licha ya maafisa wa Washington kukiri kwamba, kushikiliwa watoto hao wahajiri katika jela za nchi hiyo kunawasababishia matatizo mengi ya kimwili na kisaikolojia, lakini serikali ya Donald Trump imezidisha sera zake kali dhidi ya wahajiri na kuongeza muda wa kuwashikilia watoto hao gerezani.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza bayana kuwa, hatua ya serikali ya Marekani ya kuwatenganisha watoto wa wahajiri na wazazi wao katika mpaka wa Mexico ni ya kikatili na haikubaliki.