Mogherini: Tunafanya juhudi za kulinda mshikamano wa pande za JCPOA
(last modified Thu, 28 Nov 2019 07:38:40 GMT )
Nov 28, 2019 07:38 UTC
  • Mogherini: Tunafanya juhudi za kulinda mshikamano wa pande za JCPOA

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, amesisitizia haja ya kulindwa umoja na mshikamano baina ya pande zilizobakia katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Shirika la habari la Mehr limemnukuu Bi Federica Mogherini, akisema hayo jana mbele ya Bunge la Ulaya na kuongeza kuwa, umoja huo bado una imani na thamani za kidiplomasia na kiusalama za mapatano ya nyuklia ya JCPOA na unafanya juhudi za kulinda mshikamano kati ya pande zilizobakia kwenye makubaliano hayo ya kimataifa.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Ulaya amegusia pia fujo na machafuko yaliyotokea hivi karibuni nchini Iran na kusema kuwa, jambo hilo halina uhusiano wowote na utekelezaji wa mapatano ya nyuklia na Iran, na wala halipaswi kuwa na uhusiano wowote ule na makubaliano hayo.

Pande zilizofikia mapatano ya nyuklia ya JCPOA

 

Matamshi hayo ya Mogherini yamekuja katika hali ambayo, nchi za Ulaya zimeshindwa kuchukua hatua yoyote ya maana tangu mwezi Mei 2018, wakati rais wa Marekani, Donald Trump alipotangaza kuitoa nchi yake kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA yaliyofikiwa baina ya Iran na kundi la 5+1 na baada ya Trump kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa mapatano hayo.

Ni wajibu wa nchi za Ulaya kutekeleza kivitendo ahadi zao ndani ya makubaliano hayo ya JCPOA, lakini hadi hivi sasa zimeshindwa kutekeleza ahadi yoyote ile.

Tags