Jamii ya kimataifa yapinga hukumu ya kimaonyesho kuhusu mauaji ya Khashoggi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i58072-jamii_ya_kimataifa_yapinga_hukumu_ya_kimaonyesho_kuhusu_mauaji_ya_khashoggi
Umoja wa Mataifa umetilia mkazo udharura wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Dec 24, 2019 03:09 UTC
  • Jamii ya kimataifa yapinga hukumu ya kimaonyesho kuhusu mauaji ya Khashoggi

Umoja wa Mataifa umetilia mkazo udharura wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu mauaji ya mwandishi na mkosoaji wa utawala wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi.

Taarifa hiyo imetolewa baada ya mahakama ya Saudia kuwahukumu kifo watu watano kwa kile kilichotajwa kuwa ni kuhusika moja kwa moja na mauaji ya mwandishi huyo. Mahakama hiyo  imewaachia huru wahusika wakuu watatu katika mauaji ya Khashoggi yaliyofanyika ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki.

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stefan Dujaric amesema kuwa Antonio Guterres anasisitiza udharura wa kufanyika uchunguzi huru na usiopendelea upande wowote kuhusu watu waliohusika na mauaji hayo.

Wakati huo huo mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anayefuatilia hukumu zisizofuata sheria na mauaji ya kiholela, Agnes Callamard amesema kuwa, hukumu iliyotolewa na mahakama ya Saudia kuhusu mauaji ya Khashoggi ni kejeli na maskhara na kuongeza kuwa, wahusika wakuu wa mauaji hayo wameachiwa huru na hawakuguswa katika uchunguzi na hukumu iliyotolewa.

Vilevile msemaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch amesema kuwa hukumu iliyotolewa haikutekeleza uadilifu na kusisitiza kuwa, kesi ya mauaji ya Jamal Khashoggi ingali inagubikwa na usiri mkubwa tangu mwanzoni mwake.

Wakati huo huo mkurugenzi wa masuala ya utafiti wa Amnesty International Lyne Maalouf amesema kuwa, hukumu hii imetolewa kwa lengo la kuwasafisha wahusika halisi wa mauaji hayo na si kutimiza haki na uadilifu. Maalouf amesema hukumu hiyo si ya kiadilifu.

Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya Upelelezi ya Kongresi ya Marekani Adam Schiff amesema kuwa, hukumu ya mahakama ya Saudia kuhusu mauaji ya Khashoggi ni mwendelezo wa juhudi za kuwasafisha watawala wa Saudi Arabia akiwemo mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman na mauaji ya kutisha ya Jamal Khashoggi. Schiff ameongeza kuwa mauaji hayo yalifanyika kwa makusudi na mpangilio maalumu.

Itakumbukwa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA na nchi za Magharibi zilisema kuwa Mohammed bin Salman ndiye aliyeamuru mauaji hayo.