Wanasheria wataka rais wa Misri atiwe mbaroni mjini London
Kundi moja la mawakili wa Uingereza limetaka rais wa Misri atiwe mbaroni mara atakapofika mjini London.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu la nchini Uturuki, hivi sasa Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri ana mpango wa kufanya ziara ya siku mbili mjini London Uingereza. Mawakili hoa walioko chini ya taasisi ya "Guernica 37 International Justice Chambers" jana Jumatatu waliitaka serikali ya Uingereza itoe waranti wa kutiwa mbaroni Abdel Fattah el Sisi kwa tuhuma za kuhusika katika kifo cha Mohammad Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri.
Rais huyo wa Misri ataelekea London UIngereza kushiriki katika kikao cha uwekezaji cha Uingereza na Afrika.
Mawakili wa taasisi hiyo wamewataka polisi wa London na maafisa wa mahakama wa Uingereza kumtia mbaroni el Sisi ili aende akajibu tuhuma za kushiriki katika kifo cha Mohammad Morsi. Mawakili hao wanasema kuwa, mateso aliyopewa Morsi wakati akiwa korokoroni na dharau iliyooneshwa na maafisa wa serikali ya el Sisi wakati Morsi alipokuwa analalamika kuugua, ni ushahidi tosha wa kumtia hatiani Rais Abdel Fattah el Sisi.
Itakumbukwa kuwa Mohammad Morsi alipoteza fahamu akiwa mahakama mwaka 2019 na hakuzinduka tena mpaka kifo chake.
Kundi la Ikhwanul Muslimin la Misri lilisema masaa machache baada ya kutangazwa kifo cha Mosri kwamba, serikali ya el Sisi ndiyo iliyomuua kwa makusudi rais huyo wa zamani wa Misri.
Abdel Fattah el Sisi aliongoza mapinduzi ya kijeshi mwaka 2013 yaliyomtoa madarakani Mohammad Morsi na baadaye alimshikilia korokoroni hadi alipofariki dunia akiwa mikononi mwa serikali.