Katibu Mkuu wa UN: Radio ni chombo muhimu kinachounganisha jamii
https://parstoday.ir/sw/news/world-i59149-katibu_mkuu_wa_un_radio_ni_chombo_muhimu_kinachounganisha_jamii
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Radio inasalia kuwa chombo muhimu katika jamii kinachowaleta watu pamoja.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 14, 2020 08:41 UTC
  •  Katibu Mkuu wa UN:  Radio ni chombo muhimu kinachounganisha jamii

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Radio inasalia kuwa chombo muhimu katika jamii kinachowaleta watu pamoja.

Akizungumza kwa mnasaba wa Siku ya Radio Duniani ambayo huadhimishwa Februari 13, Guterres amesema katika enzi za mageuzi ya haraka ya vyombo vya habari, radio ni chombo  maalum katika kila jamii kama chanzo cha habari muhimu na taarifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Radio inatoa taswira nzuri na tofauti katika mundo na lugha yake.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres

Guterres ameongeza kuwa tunapojitahidi kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi radio ina jukumu muhimu la kueneza taarifa muhimu kuhusiana na kadhia hiyo. Aidha amesisitiza kwa kusema, “tukiwa katika siku hii ya Radio Duniani hebu tutambue uwezo wa radio katika kusaidia kujenga dunia ya amani na jumuishi.”
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO lilianzisha Siku ya Radio Duniani  mwaka 2012 mara baada ya Baraza Kuu la Unesco kutambua umuhimu wake na mwaka uliofuata Umoja wa Mataifa ukaitambua kama Siku ya Radio duniani.