Virusi vya Corona vyazidi kuenea bara Ulaya
Virusi hatari vya Corona vimeenea kwa kasi kubwa barani Ulaya katika kipindi cha wiki mbili zilizopita na kusababisha maafa makubwa barani humo.
Huku idadi ya watu walioathirika na kuaga dunia kutokana na virusi hivyo ikiendelea kuongezeka kwa kasi katika nchi za Ulaya katika kipindi cha siku 14 zilizopita na hasa magharibi mwa bara hilo, viongozi wa nchi hizo wanasema kwamba silaha pekee iliyobaki ya kukabiliana na virusi hivyo vinavyendelea kuangamiza wanadamu ni kutumia mbinu ya karantini.
Katika uwanja huo, Giuseppe Conte, Waziri Mkuu wa Italia ametia saini dikrii ya kuyaweka katika karantini baadhi ya maeneo ya kaskazaini mwa nchi hiyo yaliyo na idadi ya watu milioni 16. Italia iliyo na watu milioni 60 imetangaza kuwa watu 5,883 wameathirika na wengine 233 kupoteza maisha kutokana na virusi hivyo. Nchini Ufaransa watu 949 wameathirika na 19 kuaga dunia kutokana na maradhi hayo. Hispania imeuweka mji wa Haro ulioko kaskazini mwa nchi na ulio na watu 11,000 chini ya karantini ikiwa ni katika juhudi za kujaribu kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona.
Nchi hiyo imesajili watu 400 walioambukizwa virusi hivyo ambapo watatu kati yao wamepata nafuu na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Ujerumani imetangaza rasmi kuwa raia wake 800 wameambukizwa, na hivyo kuifanya kuwa nchi ya pili barani Ulaya iliyo na watu walioathirika zaidi baada ya Italia. Licha ya hayo nchi hiyo haijatangaza rasmi watu waliopoteza maisha kutokana na maradhi hayo.
Bila shaka maradhi hayo yameibua wasiwasi mkubwa duniani kuhusiana na athari zake hasi kwa ustawi wa uchumi kimataifa.
Kwa mujibu wa takwimu za karibuni kabisa, idadi ya watu walioathirika na virusi vya Corona duniani imepindukia watu laki moja na sita ambapo zaidi ya 3600 kati yao tayari wamekwishaaga dunia.