Ureno yazuilia mali za binti wa rais wa zamani wa Angola
Mahakama moja mjini Lisbon nchini Ureno imezuilia hisa za mfanyabiashara bilionea na binti wa rais wa zamani wa Angola, Jose Eduardo dos Santos, anaeandamwa na tuhuma za ufisadi.
Shirika la mawasiliano la Sonaecom jana jioni liliripoti kuwa, mahakama mjini Lisbon imezuilia hisa za shirika la NOS, linalomilikiwa na Sonaecom pamoja na Isabel dos Santos, binti wa zamani wa rais wa Angola.
Sonaecom na Isabel dos Santos wanamiliki kila mmoja asilimia 50 ya hisa za shirika la ZOPT ambalo kwa pamoja linamiliki asilimia 52.15 ya hisa za shirika la mawasiliano la NOS la Ureno.
Disemba mwaka jana, mahakama za Angola zilitangaza pia habari za kuzuiliwa akaunti za benki na mali za binti huyo wa rais wa zamani wa nchi hiyo, zikiwemo hisa alizonazo katika mashirika mbalimbali nchini humo, likiwemo shirika la mafuta la Galp.
Mapema mwaka huu, vyombo kadhaa vya habari vya ndani na nje ya Angola vilichapisha mamia ya maelfu ya nyaraka zilizofichuliwa na Jumuiya ya Kimataifa ya Wanahabari Wapekuzi (ICIJ) kuhusu namna Isabel dos Santos alivyofyonza utajiri wa nchi hiyo, wakati babake akiwa rais.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Angola mara kadhaa amezungumzia kuhusu uwezekano wa kutolewa waranti wa kukamatwa na kurejeshwa nchini watuhumiwa wa ufisadi akiwemo Isabel dos Santos, iwapo wataendelea kupuuza mwito wa kurejea nchini kwa khiari.