Aug 15, 2024 07:43 UTC
  • Israel inashinikiza ICC ifute waranti wa kukamatwa Netanyahu

Utawala wa Kizayuni umeripotiwa kushadidisha 'mashinikizo ya kidiplomasia' dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ambayo inataka kutolewa waranti wa kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na waziri wa vita wa utawala huo haramu, Yoav Gallant, kwa sababu ya kuhusika na uhalifu wa kivita.

Gazeti la Kizayuni la Ha'aretz liliripoti hayo jana Jumatano, likinukuu vyanzo rasmi na wataalamu wa sheria wakisema kuwa utawala huo umezidisha mashinikizo hayo kupitia waitifaki wake.

Ripoti hiyo imesema, kwa ombi la utawala wa Kizayuni, nchi waitifaki wa Tel Aviv zimeiandikia waraka ICC, zikisema mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Hague haina "mamlaka" ya kutoa uamuzi katika kesi hiyo. Nchi ambazo zimepinga mamlaka ya ICC kuhusu faili hilo ni pamoja na Marekani, mfadhili mkuu wa Israel, na Ujerumani.

Hii ni katika hali ambayo, nchi nyingi duniani, ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Afrika Kusini, Colombia na hata Palestina yenyewe, zimekuwa zikiishinikiza mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imkamate Netanyahu kwa kuhusika na jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza.

Mahakama ya ICC yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi

Hivi karibuni, viongozi mbali mbali wa Marekani akiwemo Rais Joe Biden walikosoa vikali ombi la Karim Khan, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC la kutaka kutolewa waranti dhidi ya Netanyahu na Gallant.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa, zaidi ya jinai 3,486 zimefanywa na Wazayuni katika kipindi cha miezi 10 iliyopita huko Gaza ambapo kutokana na jinai hizo, Wapalestina karibu 40,000 wameuawa shahidi huku hatima ya takriban watu elfu 10 ikiwa haijulikani.

Tags