Tahadhari ya maafisa wa Italia kuhusu uwezekano wa kusambaratika EU
(last modified Tue, 14 Apr 2020 06:29:07 GMT )
Apr 14, 2020 06:29 UTC
  • Tahadhari ya maafisa wa Italia kuhusu uwezekano wa kusambaratika EU

Maambukizi ya virusi vya corona na kutokuwepo ushirikiano kwa ajili ya kudhibiti kasi ya maambukizi ya virusi hivyo katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya (EU) vimetia mashakani mustakbali wa umoja huo na malengo ya kuasisiwa kwake.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wqa Kimataifa wa Italia Luigi Di Maio amezungumzia kasi ya maambukizi ya virusi vya corona nchini humo na jinsi Umoja wa Ulaya ulivyoamiliana na janga hilo na ameutahadharisha umoja huo kwamba, iwapo Italia itasambaratika, nchi zote za Ulaya pia zitasambaratika. 

Umoja wa Ulaya ambao kwa miongo kadhaa umekuwa ukifanya jitihada za kutekeleza kaulimbiu ya siasa za pande kadhaa na harakati ya kutetea maslahi ya Ulaya moja na kuliarifisha bara hilo kuwa moja ya nguvu kubwa katika medani ya kimataifa, katika miaka ya hivi karibuni hususan baada ya kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya, Januari mwaka huu, umekabiliwa na mgogoro na mgawanyiko mkubwa. Kwa kadiri kwamba, baadhi ya nchi wanachama ikiwemo Italia, zimekuwa zikijadili sana maudhui ya kujiondoa katika umoja huo. Hata hivyo masharti magumu ya kujiondoa katika Umoja wa Ulaya kwa upande mmoja na suala na kunufaika na faida za kuwepo katika umoja huo katika upande mwingine vinazizuia nchi hizo kujiondoa katika umoja huo. 

Mlipuko wa virusi vya corona barani Ulaya katika miezi ya hivi karibuni hususan wimbi ya virusi hivyo katika nchi za Italia na Uhispania na kutokuwepo ushirikiano wala msaada wa nchi nyingine za Ulaya kwa nchi hizo katika kupambana na janga hilo, vimezidisha ukosoaji mkubwa dhidi ya utendaji wa viongozi wa nchi za bara hilo. 

Mwanzoni mwa mlipuko wa virusi vya corona huko Italia na Uhispania, nchi za Ufaransa na Ujerumani zilizuia uuzaji nje wa zana na vifaa vya tiba na kuchukua uamuzi wa kufunga mipaka yao. Paris na Berlin pia zilipuuza ombi la msaada la maafisa wa Italia na Uhispania kiasi kwamba nchi za Russia na China ziliingilia kati na kutuma misaada ya zana na vifaa vya tiba kwa nchi hizo. Hali hii imeamsha hasira kali ya maafisa wa Italia na Uhispania. 

Maelfu ya watu wameaga dunia barani Ulaya kutokana na virusi vya corona

Kuendelea kwa mgogoro wa virusi vya corona, kufungwa viwanda na taasisi za uzalishaji, mdororo wa kiuchumi, kuongezeka idadi ya watu wasio na ajira na kadhalika vimezidisha mgawanyiko baina ya viongozi wa nchi za Ulaya. Hitilafu hizo zimeonekana waziwazi wakati wa kupasishwa kifurushi cha Yuro bilioni 500 kwa ajili ya kukabiliana na taathira mbaya za maambukizi ya virusi vya corona. Maafisa wa Uholanzi walitaka kuwekwa masharti kwa ajili ya kupata msaada wa kifurushi hicho ikiwa ni pamoja na sharti la kutekeleza sera za kubana matumizi ya kiuchumi. Hata hivyo hatimaye kifurushi hicho kimepasishwa kwa mashinikizo ya Ufaransa na Ujerumani. 

Pamoja na hayo na hata baada ya kupasishwa kifurushi hicho, nchi kama Italia zimesema kiwango hicho hakitoshi na zimeeleza wasiwasi wao kuhusiana na ugawaji wa kiadili wa fedha hizo.

Katika mkondo huo huo msemaji wa serikali ya Uhispania María Jesús Montero ametahadharisha kuwa, iwapo Umoja wa Ulaya hautaweza kuchukua hatua za pamoja kwa ajili ya kupambana ipasavyo na maambukizi ya virusi vya corona, watu wa Ulaya watapoteza imani yao kwa Umoja wa Ulaya. 

Kushadidi hitilafu ndani ya Umoja wa Ulaya kumeyapa makundi ya mrengo wa kulia fursa ya kuzidisha harakati zao na hata nara za kutaka kujitenga. Mrengo huo ambao unatajwa na viongozi wa nchi za Ulaya kuwa ni hatari kubwa kwa Ulaya moja, unatumia anga ya sasa kwa ajili ya kuzidisha harakati zake na unafanya jitihada za kupata wanachama wengi zaidi hususan kwa kutilia maanani kwamba, nchi kadhaa za bara hilo kama Ujerumani zinakaribia kuingia katika chaguzi. 

Akizungumzia hatari ya makundi hayo ya mrengo wa kulia, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema: Mojawapo ya njia za kukabiliana na changamoto za makundi ya mrengo wa kulia ni kutilia maanani zaidi suala ya ushirikiano na mshikamano.

Angela Merkel

Kwa sasa inatupasa kusema kuwa, Umoja wa Ulaya unakabiliwa na mtihani na kibarua kigumu. Mlipuko wa virusi vya corona umekuwa changamoto kubwa sana na unatishia umoja na mustakbali wa umoja huo. Suala hili linazidisha udharura wa kufanyika juhudi kubwa zaidi za kuimarisha na kulinda umoja huo.