Wamarekani waandamana baada ya kuchoshwa na kukaa majumbani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60467-wamarekani_waandamana_baada_ya_kuchoshwa_na_kukaa_majumbani
Mamia ya wananchi wa Marekani wamefanya maandamano katika miji na majimbo kadhaa kushinikiza kuondolewa kwa agizo la kuwataka wasalie majumbani mwao, kama njia ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2020 03:17 UTC
  • Wamarekani waandamana baada ya kuchoshwa na kukaa majumbani

Mamia ya wananchi wa Marekani wamefanya maandamano katika miji na majimbo kadhaa kushinikiza kuondolewa kwa agizo la kuwataka wasalie majumbani mwao, kama njia ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona.

Mamia ya wananchi wa Marekani waliochoshwa na agizo hilo la kutotoka nje wameandamana katika mji wa Concord jimbo la New Hampshire,  Annapolis, na Texas.

Maandamano kama haya ya kutaka kuondolewa vikwazo vya kutoka nje kwa ajili ya kuzuia maambukizo ya virusi vya Corona nchini Marekani yalishuhudiwa siku chache zilizopita pia katika majimbo ya Minnesota, Michigan na Virginia.

Duru za habari zinaarifu kuwa, akthari ya walioshiriki maandamano hayo baadhi yao wakiwa wamebeba silaha za moto ni wafuasi wa chama tawala cha Republican. Rais Donald Trump amekuwa akivutana na magavana wa majimbo ya Marekani kuhusu suala la kufungua uchumi na shughuli za kila siku za nchi hiyo.

Picha ya Wamarekani wakiandamana katika gazeti la Washington Post

Magavana na watalaamu wa afya wa Marekani wamekuwa wakipiga azma ya Trump ya kuondolewa haraka iwezekanavyo vizingiti vya kiuchumi na kijamii, akiwa na lengo la kufanya kampeni za kutaka kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu wa Novemba mwaka huu.

Hii ni katika hali ambayo, idadi ya watu waliombukizwa virusi vya Corona nchini Marekani imepindukia 740,000 huku zaidi ya 38,000 wakiaga dunia kwa ugonjwa huo na kuifanya nchi hiyo kuwa ndio iliyoathiriwa zaidi na virusi hivyo duniani.

Maandamano mengine yameshuhudiwa mjini New York, ambapo waandamanaji wamemwaga mifuko ya plastiki ya kufunga maiti nje ya Hoteli ya Trump, kulalamikia namna serikali yake imeshughulikia vibaya janga la Corona.