Kusambaratishwa njama ya kigadi dhidi ya serikali ya Venezuela
(last modified Tue, 05 May 2020 09:18:26 GMT )
May 05, 2020 09:18 UTC
  • Kusambaratishwa njama ya kigadi dhidi ya serikali ya Venezuela

Katika mwendelezo wa njama za Marekani na washirika wake za kutaka kuiangusha serikali ya Rais Nicolas Maduro wa Venezuela, maafisa wa nchi hiyo wametangaza kuwa, wamefanikiwa kusambaratishwa operesheni moja ya kigaidi sambamba na kuangamizwa magaidi ambao walikuwa wanakusudia kupenya ndani ya nchi hiyo kupitia baharini.

Néstor Reverol, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela amesema: Kundi la mamluki magaidi lililotokea Colombia, lilikusudia kufanya mauaji dhidi ya viongozi wa ngazi ya juu wa serikali na kuendesha vitendo vya ukatili ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini. Hata hivyo, hatua ya haraka na iliyochukuliwa kwa wakati ya vikosi vya ulinzi vya Venezuela imesambaratisha njama hiyo ya kigaidi ambapo maafisa wa ulinzi wamewaua baadhi ya magaidi hao na kuwatia mbaroni wengine kadhaa ambapo baadhi yao ni raia wa Marekani.

Viongozi wa Venezuela wanasema kuwa, wamefanikiwa kukamata vyombo vya mawasiliano kwa njia ya satalaiti, nyaraka, silaha za kisasa na unifomu pamoja na kofia ambazo zimeshonwa kwa kitambaa cha bendera ya Marekani. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela amewataja wafanya hujuma hiyo kuwa ni “magaidi wa kukodishwa” ambao wanafanya njama za kuvuruga amani na uthabiti wa nchi hiyo.

Moja ya mashinikizo ya Marekani dhidi ya Venezuela ni kuiwekea vikwazo nchi hiyo ya Amerika ya Latini

Ni kwa miaka mingi sasa ambapo Venezuela imekuwa ikiandamwa kwa mashinikizo makubwa zaidi ya Marekani. Kimsingi ni kuwa, viongozi wa Marekani wamekuwa wakifanya kila wawezalo ili kuziondoa madarakani serikali za mrengo wa kushoto katika eneo la Amerika ya Latini. Siasa hizo za Marekani zimeshadidi zaidi tangu Rais Donald Trump aliposhika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Trump amekuwa akiendesha siasa za chuki na kufanya njama za kuwaondoa madarakani viongozi wa serikali za mrengo wa kushoto katika eneo hilo la Amerika ya Latini, ambazo zinakwenda kinyume na matakwa pamoja na maslahi ya Washington.

Viongozi wa Marekani wanafanya njama za kuiondoa serikali ya mrengo wa kushoto nchini Venezuela na badala yake waiweke madarakani serikali ambayo ni mfuasi na tiifu kwa Washington na ambayo itadhamini na kutekeleza amri na maagizo ya Washington. Katika uwanja huo, kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa ambapo Marekani imekuwa ikimuunga mkono Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela ambaye mwaka jana alijitangaza kuwa Rais wa Venezuela.

Ili kufikia lengo lake hilo, Marekani imekuwa ikitekeleza siasa mbalimbali dhidi ya Venezuela kama mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa, kuziwekea vikwazo vizito sekta mbalimbali za uchumi wa nchi hiyo, kutekeleza majaribio ya mapinduzi na kuwaunga mkono wafanya mapinduzi.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela anayeungwa mkono na Marekani

Ukweli wa mambo ni kuwa, sera za tawala za mrengo wa kushoto katika Ukanda wa Amerika ya Latini ikiwemo Venezuela na Cuba haziwafurahishi hata kidogo viongozi wa Marekani. Mataifa hayo, yangali yanafungamana na malengo kama ya kupigania uadilifu, mapambano dhidi ya ukoloni na kukabiliana na ubeberu na hayako tayari kuzifanya harakati zao za kupigania uhuru kuwa mhanga wa siasa za Washington.

Fernandez Pascualino, Katibu Mkuu wa Baraza la Ulinzi la Venezuela sanjari na kuashiria kwamba, Marekani daima imekuwa ikikodolea macho ya tamaa utajiri na rasilimali za Venezuela na ndio maana imeanzisha vita hivi vya pande kadhaa dhidi ya nchi hii amesema kuwa: Marekani ni kama utawala ambao unataka kupora vyanzo vyote vya utajiri vya Venezuela na hii ndio sababu na chimbuko la hitilafu zote.

Katika miezi ya hivi karibuni, Marekani na washirika wake wameshadidisha njama za kufanya mapinduzi nchini Venezuela kupitia mipango mbalimbali kiasi kwamba, Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo ametahadharisha mara chungu nzima kuhusiana na kufanyika majaribio mengi ya kutaka kumuondoa madarakani.

Maandamano ya wananchi ya kuitaka serikali ya Marekani ikomeshe njama zake dhidi ya Venezuela

Hata hivyo licha ya njama zote hizo za Marekani na hatua yake ya kuwaunga mkono wapinzani wa Venezuela, lakini Washington imeshindwa kufikia malengo yake. Himaya na uungaji mkono wa wananchi na jeshi kwa Rais Maduro na hitilafu za kimitazamo baina ya wapinzani wa Maduro kuhusiana na kumtambua rasmi Juan Guaido ni miongoni mwa sababu ambazo hadi sasa zimepelekea kufeli njama na majaribio yote ya mapinduzi dhidi ya Rais Maduro.

Hata hivyo, pamoja na kushindwa kote huko, lakini Marekani haiakata tamaa kwani ingali inaendelea na njama zake za kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro. Hata hivyo inaonekana kuwa, madhali serikali ya Maduro ingali inaungwa mkono na wananchi, njama na hatua zozote zile za serikali ya Trump za kutaka kumuondoa madarakani kiongozi huyo waVenezuela hazitazaa matunda.

Tags