Russia: Marekani ilifanya kosa la kistratijia kujiondoa JCPOA
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Wizara ya Ulinzi ya Russia amesema kuwa viongozi wa Marekani hawana uwezo wa kuandaa mazingira ya kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.
Igor Korotchenko, mjumbe wa Baraza la Kijamii la Wizara ya Ulinzi ya Russia amebainisha kwamba miaka miwili baada ya kujiondoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Marekani haijafikia malengo yake ya kuishinikiza Iran ibadili siasa zake. Amesema kuwa ikiwa imebakia miezi sita kabla ya kumalizika muda wa vikwazo vya silaha iliyowekewa Tehran, Washington imejikuta tena katika mtihani mgumu kwa kujaribu kuandaa mazingira ya kurefushwa vikwazo hivyo. Igor Korotchenko ameongeza kuwa, huku ikiwa imesalia miezi michache kabla kufanyika uchaguzi wa rais wa 2020 nchini Marekani, watawala wa Republican nchini humo wakiongozwa na Rais Donald Trump hawajaweza kufikia malengo yao ya kisiasa kuihusu Tehran na badala yake wamejikuta wakiwa mikono mitupu.
Afisa huyo wa ngazi ya juu katika Wizara ya Ulinzi ya Russia amebainisha kuwa, kitendo cha Washington kusisitiza kutumia azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kurefusha vikwazo vya silaha baada ya mwezi Oktoba mwaka huu dhidi ya Iran, ni aina ya ubeberu wa kisiasa ambao hauna uhalali wowote wa kisheria. Amemalizia kwa kusema kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani alichukua hatua mbovu ya kuiondoa nchi yake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA miaka miwili iliyopita na kwa sasa hana ruhusa wala hiari yoyote katika uwanja huo kwa kuwa Washington sio mwanachama tena wa JCPOA.