Russia: Hatuitaruhusu Marekani irefushe vikwazo vya silaha dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i60953-russia_hatuitaruhusu_marekani_irefushe_vikwazo_vya_silaha_dhidi_ya_iran
Russia imesema itapinga jitihada zozote za Marekani za kutaka muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran uongezwe utakapomalizika mwezi Oktoba mwaka huu.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
May 13, 2020 03:48 UTC
  • Russia: Hatuitaruhusu Marekani irefushe vikwazo vya silaha dhidi ya Iran

Russia imesema itapinga jitihada zozote za Marekani za kutaka muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran uongezwe utakapomalizika mwezi Oktoba mwaka huu.

Hayo yalisemwa jana Jumanne na Vassily Nebenzia, Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa ambaye anasisitiza kuwa, "vikwazo hivyo vya silaha (dhidi ya Iran) vinafikia tamati mwezi Oktoba na sioni sababu yoyote ya kuvirefusha. Moscow haitaruhusu jambo hilo kufanyika."

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, Marekani ilisambaza rasimu ya azimio la kutaka vikwazo hivyo vya silaha dhidi ya Iran virefushwa kwa muda usiojulikana katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini inatarajiwa kuwa Russia itatumia kura yake ya turufu (veto) kupinga azimio hilo. 

Kabla ya hapo, Mikhail Ivanovich Ulyanov, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Russia katika asasi za kimataifa  zenye makao yake mjini Vienna Austria ameashiria juhudi za Marekani za kutaka kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Kutakuwa na kibarua kigumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na jambo hilo.

Baraza la Usalama la UN

Baada ya kupasishwa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2015, suala la kuipatia Iran aina saba za zana za kivita lilipigwa marufuku.

Baadhi ya zana hizo ni ndege za kivita, manowari za kivita, makombora, magari ya deraya na vifaa vya mizinga. Marufuku hiyo ya sasa ya kuiuzia Iran au Iran yenyewe kuuza silaha hizo inatarajiwa kufikia tamati Oktoba 18 mwaka huu.