Mvutano usio wa kawaida katika Rasi ya Korea
(last modified Wed, 17 Jun 2020 07:16:42 GMT )
Jun 17, 2020 07:16 UTC
  • Mvutano usio wa kawaida katika Rasi ya Korea

Kufuatia kuongezeka mvutano kati ya Korea mbili, Korea Kaskazini imelipua ofisi ya masuala ya kiutamaduni iliyoanzishwa kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano ya nchi mbili katika eneo la viwanda la Kaye Sung.

Ofisi hiyo ililipuliwa jana alasiri kwa wakati wa Korea Kusini. Licha ya kuwa Korea Kaskazini haijathibitisha kuhusika kwake katika ulipuliwaji wa ofisi hiyo ya mawasiliano lakini katika siku za karibuni viongozi wa nchi hiyo wamekuwa wakitoa vitisho vya kuiharibu. Ofisi hiyo ilianzishwa mwaka 2018 kufuatia juhudi kubwa zilizofanywa na viongozi wa nchi mbili kwa lengo la kupunguza mivutano iliyokuwepo wakati huo. Ofisi hiyo imekuwa muhanga wa kuongezeka mivutano ya kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi kati ya nchi mbili katika siku za hivi karibuni.

Katika kipindi cha miaka miwili ambapo viongozi wa Korea Kaskazini na Kusini walikuwa wamefanya juhudi kubwa za kidiplomasia kwa madhumuni ya kuondoa tofauti na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hizi jirani, swali linaloulizwa ni kuwa je, ni nini ambacho kimevuruga juhudi hizo na kuzirejesha nchi hizo katika mivutano na uhasama wa zamani?

Viongozi wa Korea mbili wakijaribu kuimarisha usalama na amani ya nchi zao

Suala lisilo na shaka ni kwamba Korea Kaskazini imechukua hatua ya kulipua ofisi hiyo ya mawasiliano ya nchi mbili kutokana na hatua kadhaa za kichochezi ambazo zimetekelezwa na Korea Kusini katika siku za karibuni. Kuongezeka harakati za wapinzani wa serikali ya Korea Kaskazini katika ardhi ya Korea Kusini zikiwemo za kurusha angani karibu na mpaka wa Korea Kaskazini, maputo yaliyo na nara za kichochezi na kipropaganda dhidi ya serikali ya Pyongyang kwa upande mmoja na ushirikiano wa Soul na Washington kwa ajili ya kuzindua mfumo wa ulinzi wa makombora wa THAAD kwa upande wa pili, ni mambo yaliyowakera sana viongozi wa Korea Kaskazini. Hatua zingine za kichochezi ambazo viongozi wa Pyongyang wanazichukulia kuwa za kichokozi na zinazohatarisha usalama wake wa kitaifa ni kuhamishwa wanajeshi wa Marekani kutoka kambi za kijeshi zilizoko katika viunga vya mji wa Seoul na kupelekwa katika vituo vikubwa na vya kisasa kabisa na pia ushirikiano wa Korea Kusini na Washington katika kutekeleza vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Korea Kaskazini. Mambo hayo yamewapeleka viongozi wa Korea Kaskazini kufikia uamuzi huu kuwa Korea Kusini na Marekani hazina nia yoyote ya kuimarisha usalama katika Rasi ya Korea.

Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kuwa hatua hizo zote zimechukuliwa katika kipindi cha kukwama mazungumzo ya Korea Kaskazini na Marekani katika miezi iliyopita. Hali hiyo imewathibitishia Wakorea Kaskazini kwamba Seoul, na kutokana na mashinikizo ya Marekani, haina nia ya kuchukua misimamo huru katika kuimarisha uhusiano wake na Pyongyang wala kutekeleza ahadi ilizotoa huko nyuma kuhusiana na suala hilo.

Kulipuliwa ofisi ya mawasiliano ya kiutamaduni ya nchi mbili katika eneo la Kaye Sung si tu kwamba kunazirejesha nchi mbili hizo jirani katika kipindi cha mivutano mingi bali pia kunafunga mlango wa mazungumzo yaliyokuwa yameanzishwa na Korea Kaskazini na Marekani huko Singapore mwaka 2018. Inavyoonekana, na kama walivyosisistiza mara nyingi viongozi wa Korea Kaskazini, ni kuwa nchi hiyo sasa itaendelea kujiimarisha kijeshi na kutegemea uwezo wake wa ndani katika kulinda maslahi na kukidhi mahitaji ya nchi hiyo ya Asia.

Rais Trump wa Marekani akiwa na askari wa nchi yake walioko Korea Kusini

Matamshi ya viongozi wa Korea Kaskazini katika wiki za karibuni yanathibitisha wazi kwamba subira yao imefika ukingoni kutokana na uvunjaji ahadi wa Marekani na mbinu za kupoteza wakati za viongozi wa Seoul.

Nukta isiyopasa kusahaulika hapa ni hatua haribifu zinazochukuliwa na Marekani na washirika wake wa eneo katika kuvuruga kila juhudi zinazofanywa na Korea mbili kwa lengo la kuleta amani kati yao. Kila mara nchi hizo zilipofanya juhudi za kuimarisha amani kati yao katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, viongozi wa kisiasa katika miji ya Tokyo na Washington wameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusiana na suala hilo.

Ukweli wa mambo ni kuwa kwa miongo kadhaa sasa, Marekani imekuwa ikitumia kisingizio cha 'tishio la Korea Kaskazini' kuendelea kubakisha makumi ya maelfu ya askari wake katika eneo la Rasi ya Korea. Hivyo iwapo amani itapatikana huko ni wazi kuwa nchi hiyo ya Magharibi haitakuwa tena na kisingizio cha kuendela kubakisha askari wake katika eneo hilo. Kwa msingi huo ni jambo lisilo na shaka kuwa Marekani haijakuwa na nia yoyote ya kuleta amani katika eneo hilo nyeti la Rasi ya Korea. Japan nayo haitaki nchi mbili hizo ziishi katika mazingira ya amani kutokana na mashindano yake ya kale na Korea Kusini.

Hivyo katika kutathmini mivutano kati ya Korea mbili tunapasa pia kuzingatia masuala yaliyo nje ya mipaka ya nchi hizo na nafasi haribifu inayotekelezwa na nchi zilizo nje ya Rasi ya Korea kwa madhara ya majirani hao wawili.

Tags