Aug 15, 2024 02:43 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 15 Agosti, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Safar 1446 Hijria inayosadifiana na Agosti 15 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, mfereji wa Panama ulifunguliwa rasmi kufuatia kupita meli ya kwanza katika kanali hiyo. 

Ujenzi wa kanali hiyo ulianzishwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye serikali ya Marekani ilinunua kampuni ya Ufaransa iliyokuwa ikijenga mfereji huo na kukamilisha ujenzi wake.

Kujengwa mfereji huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 60 kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic.   

Miaka 77 iliyopita India ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza, baada ya miaka mingi ya mapambano ya kupigania uhuru.

India ina historia kongwe na watawala mbalimbali wa ndani na nje wamewahi kutawala nchini humo.

Mapambano ya wananchi wa India dhidi ya mkoloni Muingereza yalipamba moto zaidi baada ya kuasisiwa Chama cha Congress ya Kitaifa na kujiunga na chama hicho Mahatma Gandhi.     

Miaka 76 iliyopita, sawa na tarehe 15 Agosti 1948 nchi ya Korea ya Kusini iliundwa baada ya kujitokeza mgawanyiko wa visiwa vya Korea.

Visiwa vya Korea vilikabiliwa na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu wa madola yenye nguvu katika eneo hilo kama vile China na Japan tokea nusu ya kwanza ya karne ya ishirini.   

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alikimbilia Italia akiwa pamoja na mkewe.

Kabla ya kuikimbia Iran, Muhammad Reza Pahlavi alitia saini hukumu ya kuuzuliwa Waziri Mkuu, Muhammad Musaddiq, na alikimbia Italia baada ya kutambua kuwa, kulikuwepo mpango wa kufanyika mapinduzi dhidi yake. Wakati huo Musaddiq alikuwa ametaifisha sekta ya mafuta, suala ambalo lilihatarisha maslahi ya Uingereza nchini Iran.

Siku tatu baadaye dola hilo la kikoloni lilitekeleza mapinduzi dhidi ya serikali ya Dokta Musaddiq na kumrejesha nchini dikteta na kibaraka wake, Shah Pahlavi ambaye aliitawala Iran hadi mwaka 1979 wakati Mapinduzi ya Kiislamu yaliyoongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini yalipopata ushindi na kuzika kabisa utawala wa kifalme hapa nchini.

Muhammad Reza Pahlavi

Miaka 64 iliyopita katika siku kama hii ya leo nchi ya Jamhuri ya Congo Brazzaville ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa.

Huko nyuma Congo Brazzaville ilikuwa sehemu ya ardhi ya Congo katika Afrika Magharibi iliyojumuisha Zaire ya zamani na Angola.  

Kongo Brazzaville iligunduliwa na Wareno katika karne ya 15 na baadaye ilikaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kifaransa kwa miaka kadhaa mfululizo. Kongo Brazaville iko magharibi mwa Afrika ikipakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola.     

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 25 Mordad 1372 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 16 Agosti mwaka 1993 alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari mwanachuoni mashuhuri wa nchini Iran.

Ayatullah Sabzawari alizaliwa mnamo mwaka 1290 Hijiria Shamsia, sawa na mwaka 1911 Miladia, katika mji huo uliopo kaskazini mashariki mwa Iran. Mwanachuoni huyo licha ya kujipatia elimu zake za msingi katika mji wa Sabzawar na kisha kusoma elimu ya dini mjini Mash’had, alielekea Najaf nchin Iraq na kujipatia elimu ya juu ya maarifa ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari ameandika vitabu tofauti maarufu zaidi ikiwa ni pamoja na vitabu vya ‘Mawaahibul-Rahman fii Tafsirul-Qur’an’ chenye juzuu 20, ‘Muhadh-Dhibul-Ahkaam fii Bayaanil-Halali wal-Haraam’ chenye juzuu 30 na ‘Tahdhibul-Usulu’ chenye juzuu mbili.

Ayatullah Sayyid Abdul-A'alaa Mussawi Sabzawari

 

Na siku kama hii ya leo miaka 19 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Agosti 2005, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kuondoka katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Eneo hilo lilikaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1967, baada ya kutokea vita vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel. Lakini pamoja na hayo utawala huo katili hutekeleza mashambulio ya mara kwa mara dhidi ya Gaza na kuwaua Wapalestina wengi hasa  wanawake na watoto.

 

Tags