Aug 04, 2020 06:49 UTC
  • Russia yajibu vitisho vya makombora vya Marekani

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russia imetangaza kuwa, nchi hiyo haitafumbia jicho vitisho vya makombora ya Marekani.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russia kwa mnasaba wa hatua ya Marekani ya kujiondoa kwenye Mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) imesema kuwa, kuweka makombora ya nyuklia ya masafa mafupi na ya masafa ya kati ya Marekani katika maeneo mbalimbali duniani kunahatarisha sana amani ya kikanda na kimataifa. 

Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russian imesema kuwa, hatua hiyo ya Marekani itaanzisha awamu mpya na hatari ya mashindano ya silaha.

Taarifa hiyo imesema kuwa, Russia haiwezi kufumbia jicho vitisho zaidi vya makombora dhidi ya ardhi yake. Imesema njia pekee ya kimantiki ni kupatikana mwafaka kupitia njia za kisiasa na kidiplomasia. Imesisitiza kuwa Russia iko tayari kurejesha hali ya kuaminiana na kuimarisha amani ya kimataifa na ina matumaini kwamba, Marekani pia itachukua hatua za kimantiki na za kuwajibika katika uwanja huu. 

Hivi karibuni, Marekani ilitangaza kujitoa kwenye mkataba wa pande mbili iliosaini na Russia, wa kupiga marufuku silaha za nyuklia za masafa ya kati (INF).

Kufuatia hatua hiyo ya Marekani, Russia nayo ilijibu mapigo na kuamua kujitoa kwenye mkataba huo.

Aliyekuwa Kiongozi wa Urusi ya zamani (USSR) Mikhail Gorbachev (kushoto) na rais wa wakati huo wa Marekani Ronald Reagan wakisaini mkataba wa INF

Mnamo mwezi Juni 1987, Marekani na Urusi ya zamani zilisaini mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia za masafa ya kati INF, ambao ulianza kutekelezwa rasmi Juni 1988.

Makubaliano ya INF yalipiga marufuku Washington na Moscow kuweka makombora yao ya balestiki na cruise barani Ulaya.

Tags